Na Ismail Ngayonga - MAELEZO, Dar es Salaam
WIZARA ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wamewekeana saini ya mkataba na makampuni ya Ndovu resource na Heritage Oil kutoka nchini Uingereza kwa ajili ya uchimbaji na utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi katika Kisiwa cha Songosongo na Ziwa Rukwa.
Akizungumza katika hafla hiyo jana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema uwekaji saini wa mikataba na makampuni hayo unaifanya Tanzania kuwa na mikataba 23 na makampuni 17 ya utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Alizitaja nchi zenye makampuni hayo ni Australia, Uingereza, Ufaransa, Brazil, Norway, Marekani, Canada na Nchi za Falme ya Kiarabu.
Waziri Ngeleja alisema utiaji saini na makampuni hayo ni kielelezo cha sera nzuri zilizopo katika sekta ya nishati na hivyo kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kivutio cha uwekezaji kwa kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
“Mikataba hii imezingatia maslahi ya taifa pamoja na makampuni haya kufuata sheria za nchi yetu ikiwemo suala zima la uhifadhi wa mazingira ambalo ni jambo la msingi kwa wananchi wetu” alisema Ngeleja.
Aidha Waziri Ngeleja aliitaka TODC kusimamia vyema masharti ya mikataba hiyo ikiwemo fedha zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo ya watumishi wa shirika hilo yanayolenga kuliwezesha taifa kupata wataalamu wake wataosimamia vyema rasilimali za mafuta na gesi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Yona Killagane alisema ujio wa makampuni hayo ni fursa nzuri iliyopata Tanzania katika kufumbua vyanzo mbalimbali vya nishati ya mafuta na gesi vilivyopo nchini.
“Kabla ya kufikia hatua hii ya utiaji saini, tulichukua hatua za makusudi ili kujiridhisha kuwa mikataba hii itazingatia maslahi ya taifa” alisema Killagane.
Naye Kamishina Msaidizi wa maendeleo ya gesi na petrol katika Wizara ya Nishati na Madini, Prosper Victus alisema mikataba hiyo itagharimu kiasi cha Dola Milioni 70 na shughuli hiyo ya utafutaji wa nishati hizo za inatarajia kuchukua kipindi cha miaka 11 iliyogawanywa katika awamu 3 za utekelezaji.
Alisema kampuni ya Ndovu Resource itachimba nishati hiyo ya mafuta na gesi katika eneo la songosongo mashariki wakati kampuni ya Heritage Oil itafanya shughuli hiyo katika ziwa Rukwa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Ndovu Resource, Brian Hall alisema kampuni yake itaheshimu vipengele vya mkataba huo ikiwemo suala la uchangiaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya uchimbaji wa nishati hizo.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kampuni ya heritage Oil, Brian Smith alisema kampuni yake itahakikisha suala la ajira kwa vijana linapewa kipaumbele, kwani nia ya taasisi hiyo ni kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya umaskini kwa wananchi wake.
No comments:
Post a Comment