Friday, October 21, 2011

DR. OMAR DADI AELEZA UMUHIMU WA SERA NA MIKAKATI MADHUBUTI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak ameelezea umuhimu wa kuwepo kwa sera na mikakati madhubuti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizindua kamati ya kitaalamu ya kusimamia mabadiliko ya tabianchi Zanzibar hukoa ofisini kwake Migombani, Dr. Shajak amesema suala la mabadiliko ya tabianchi linamuhusu kila mtu na linagusa nyanja mbali mbali za kijamii zikiwemo uchumi ya afya.
Amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuunganisha nguvu zao ili kuhakikisha kuwa suala hilo linafanikiwa kwa maslahi ya wananchi ya taifa kwa jumla.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo bibi Fauzia Mwita amesema ushauri wa kitaalamu unahitajika katika kuliendeleza suala hilo, na kwamba kamati hiyo italazimika kutoa taaluma kwa wajumbe wake ili iweze kufanya kazi zake vizuri.
Nae mjumbe wa Sekretarieti ya mabadiliko ya tabianchi Zanzibar Bw. Sihaba Haji Vuai amesema mradi wa mai wa AAP unaotekelezwa katika kijiji cha Nungwi ni miongoni mwa hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hapa Zanzibar.
Amesema mradi huo utakapokamilika utaweza kuondoa tatizo la muda mrefu la wananchi wa Nungwi la ukosefu wa maji safi na salama, kwa vile maji yao yamekuwa yakichanganyika na maji ya chumvi.
Kamati hiyo ya kitaalamu inaundwa na wakurugenzi kutoka  taasisi mbali mbali zikiwemo kilimo, mazingira, maji na mamlaka ya hali ya hewa.

Hassan Hamad (OMKR). 

No comments:

Post a Comment