Friday, October 28, 2011

TATIZO LA UHARAMIA KATIKA BAHARI YA AFRIKA MASHARIKI LINALETA ATHARI KUBWA ZA KIUCHUMI - MAALIM SEIF

Maalim Seif akiagana na Waziri wa Maendeleo wa Finland Bibi Heidi Hautala baada ya kumaliza mazungumzo ofisini kwake Migombani
Maalim Seif akizungumza na Waziri wa Maendeleo wa Finland Bibi Heidi Hautala Ofisini kwake Migombani Mjini Zanzibar (Picha: Salmin Said-OMKR)

Na: Hassan Hamad (OMKR).

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema tatizo la uharamia katika bahari ya Afrika Mashariki linaleta athari kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema wafanyabiashara wamekuwa wakizungunguka masafa marefu kuwakimbia maharamia, jambo ambalo linapelekea kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na kuleta malalamiko kwa wananchi kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa mbali mbali zikiwemo za vyakula.
Maalim Seif ameeleza hayo huko Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na Waziri wa Maendeleo wa Finland bibi Heidi Hautala.
Ameiomba jamii ya kimataifa kuangalia uwezekano wa kulidhibiti suala hilo ili kuleta unafuu kwa wafanyabiashara na hatimae wananchi waweze kunufaika kwa kuweza kumudu bei za bidhaa hasa vyakula.
Amesema suala hilo linaweza kudhibitiwa iwapo jamii ya kimataifa itaweka mikakati imara ikiwa ni pamoja na kushirikiana na viongozi wa mataifa yanayokumbwa na tatizo hilo.
Akizungumzia kuhusu mazingira Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kuhifadhi rasilimali asilia zikiwemo misitu na vianzio vya maji ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa matumizi mbali mbali.
Amesema tatizo la uharibifu wa mazingira limekuwa likileta athari kubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kukosekana mvua kwa wakati pamoja na upungufu wa maji safi na salama kutokana na vianzio vyake kuharibiwa.
Kwa upande mwengine Maalim Seif amesema serikali inajipanga kusimamia udhibiti wa ardhi, ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 asilimia 50 ya ardhi iwe imesajiliwa, na kwamba hatua hiyo itasaidia kuweka mipango imara ya kutenganisha maeneo ya kilimo na yale ya makaazi.
Amefahamisha kuwa Serikali pia inazihamasisha taasisi za kijamii na zile za binafsi kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira ili jamii nayo ipate mwamko wa kutosha juu ya umuhimu wa kuyalinda mazingira yao.
Kuhusu dawa za kulevya, Maalim Seif amesema serikali inaendelea na mkakati wake wa kuwaunganisha vijana walioathirika na utumiaji wa dawa za kulevya kwa lengo la kuwasaidia kupata ajira, ili waweze kuepukana na kujishughulisha na dawa hizo.
Amesema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watu wanaojihusisha na dawa za kulevya ambapo kupitia Wizara ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi vijana wanahamasishwa kujiunga na vikundi vya ushirika ili wawezeshwe kujikwamua kiuchumi.
Amebainisha kuwa utumiaji wa dawa za kulevya unaongeza umaskini katika ngazi ya familia hadi taifa, kwa vile watumiaji hao wakati mwengine huiba vitu vya nyumbani na kuviuza kwa bei nafuu kwa dhamira ya kujitafutia mahiji yao, jambo ambalo hurejesha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo.
Nae Waziri wa biashara wa Finland bibi Heidi Hautala amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya kwani zimekuwa zikichangia uhalifu katika nchi mbali mbali.
Amesema iwapo vijana watawezeshwa kiuchumi na kupewa elimu ya kutosha juu ya janga hilo wanaweze kuachana na vitendo hivyo na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kuhusu Mazingira Waziri huyo amesema ipo haja kwa Zanzibar kuzingatia umuhimu wa matumizi bora ya Ardhi, kwani iwapo itatumika ipasavyo itasaidia harakati za maendeleo na kiuchumi kwa urahisi zaidi.
Bibi Hautala ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Finland na Zanzibar, sambamba na kuiendeleza miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na nchi hiyo  ukiwemo mradi wa uhifadhi wa ardhi na mazingira wa SMOLE.

No comments:

Post a Comment