Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Daniel Ole Njoolay akiwa na Mama Njoolay usiku wa jana alipokuwa akiagwa katika ukumbi wa Upendo View Wilayani Sumbawanga
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Daniel Ole Njoolay ameagwa rasmi jana katika ukumbi wa Upendo View uliopo wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa. Sherehe hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo ilikuwa pia ya kumkaribisha rasmi Mkuu mpya wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB).
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi pamoja na watumishi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi katika Mkoa wa Rukwa. Bw. Daniel Ole Njoolay alishukuru kwa ushirikiano aliopewa kwa kipindi chote alichokuwa madarakani akiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Alisema kuwa "Maendeleo haya ya Mkoa wa Rukwa siyo ya kwangu peke yangu bali ni yetu sote"
Zawadi mbalimbali zilitolewa kwa Mkuu wa Mkoa aliyemaliza muda wake na yule aliyechukua nafasi. Kwa upande wake Injinia Manyanya ambaye ndiye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa sasa alisema "Zawadi hizi mlizotoa hapa leo ni za aina mbili, moja ya kumpongeza Bw. Njoolay lakini ya kwangu mimi ni deni na ninaahidi kulilipa kwa kuwafanyia kazi nnachoomba kwenu ni ushirikiano".
Aliendelea kusema kuwa watu wengi huogopa kuishi ndani ya mabadiliko, akawaasa wanarukwa kutokuogopa mabadiliko na kuwasihi kuonyesha ushirikiano, kudumisha amani na kuepuka misuguano ya kisiasa kwakuwa itamuongezea mzigo usiokuwa na ulazima.
Katika hotuba yake Mkuu wa Mkoa aliyemaliza muda wake Bw. Daniel Ole Njoolay aliaga kwa kuwaachia wanarukwa changamoto nne, moja ikiwa ni elimu kwani wananchi wengi wa Rukwa elimu kwao sio kipaumbele aliwaasa wanarukwa kuikumbatia elimu.
Changamoto nyingine ni uharibifu wa mazingira hususani uchomaji moto misitu, tatizo la masoko na fursa iliyotolewa na Rais ya kuuza mazao nje itumike kutafuta masoko katika nchi jirani. Nyingine ni uboreshaji wa michango kwa ajili maendeleo ya Rukwa, Halmashauri na wadau wengine wa maendeleo wameelekea kusuasua kuchangia kitu ambacho kitazorotesha maendeleo ya Rukwa.
Alimalizia kwa kusema kuwa changamoto hizo pamoja na nyingine za miundombinu ambazo zishaanza kupatiwa ufumbuzi zikikamilika na kufanyiwa kazi ipasavyo basi kuna matuamaini makubwa kuwa katika miaka kumi (10) ijayo Mkoa wa Rukwa ndio utakaoongoza kiuchumi nchi nzima.
No comments:
Post a Comment