Sunday, October 9, 2011

SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR IMESEMA ITACHUKUA HATUA ZA HARAKA KULIPA MADENI YA GHARAMA ZA UOKOAJI ABIRIA

Na: HASSAN HAMAD (OMKR)
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itachukua hatua za haraka kulipa madeni ya gharama za ukoaji abiria zilizotumiwa na wavuvi na wawekezaji katika sekta ya utalii, baada ya kutokea ajali ya meli ya Spice Islnder Septemba 10, mwaka huu.

Ahadi hiyo imetolewa leo na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa akitoa shukurani kwa wavuvi wa Nungwi na vijiji jirani pamoja na wawekezaji walioshiriki katika uokoaji wa abiria waliokuwemo katika meli hiyo, katika mkutano uliofanyika hoteli ya Roral Zanzibar,  mkoa wa Kaskazini Unguja.

Maalim Seif alisema kazi iliyofanywa na wavuvi pamoja na wawekezaji hao hailipiki na watarajie malipo klutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa vile kuna watu waliokopwa fedha kwa ajili ya mafuta na gharama nyengine za kufanikisha kazi ya uokoaji maisha ya watu deni hilipo halinabudi kulipwa.

Ameitaka wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa mchanganuo wa gharama hizo za madeni ili kwa kushauriana na kushirikiana na  serikali yaweze kulipwa haraka.

Alisema kwamba kazi kubwa iliyofanywa na wavuvi hao katika kuokoa maisha ya binaadamu imelifanya Taifa lijivune na Serikali inajivunia ari na moyo wa hali ya juu uliooneshwa na wavuvi na wawekezaji mara baada ya kupatikana taarifa za kuzama kwa meli hiyo.

Alieleza kwamba kwa namna wavuvi na wananchi wengine wa Zanzibar walivyoshiriki katika kazi ya uokozi wa abiria hata baadhi ya mataifa yenye uzoefu katika kukabiliana na majanga kama hayo yasingeweza kufikia kiwango kama hicho.

Amesema Serikali inajipanga kuwawezesha wavuvi wa maeneo yote ya Zanzibar ili waweze kuongeza ujuzi wa uvuvi na uokozi kwa lengo na kuweza kukabiliana na maafa kama hayo wakati yanapotokea.

Mapema Maalim Seif alitembelea maeneo mbali mbali kuangalia shughuli zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo alikutana na wafugaji wadogo wadogo wa kuku huko maruhubi, na kuwataka kuongeza juhudi za uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Amesema iwapo wafugaji wataongeza uzalishaji wa kuku na mayai, Serikali itakuwa na kila sababu ya kulinda soko lake la ndani kwa lengo la kutoa ajira zaidi kwa wazalendo katika sekta ya mifugo.

No comments:

Post a Comment