Tuesday, October 11, 2011

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ITAENDELEA KUBAKI KUWA KITUO CHA HISTORIA YA UKOMBOZI KWA MATAIFA MENGI YA BARA LA AFRIKA

Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kubakia kuwa  Kituo cha Historia ya Ukombozi kwa Mataifa Mengi ya Bara la Afrika wakati yalipokuwa yakitafuta Uhuru kutoka kwa Watawala wa Mataifa hayo.

Baadhi ya Mabalozi wa Nchi za  Nje waliopo Nchini Tanzania wameeleza hayo wakati wa Tafrija ya kupongezwa kwao baada ya Kukamilisha ziara yao ya siku tatu katika maeneo tofauti ndani ya Tanzania.

Tafrija hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nchi wa Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imefanyika katika Hoteli ya Tembo iliyopo Forodhani Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Mabalozi hao wamesema Mataifa yao yataendelea kuiheshimu Tanzania kwa vile ilikuwa chachu ya Ukombozi wa Mataifa yao.

Mwenyeji wa Wanadiplomasia hao Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe amesema Tanzania itapata faida ya Kiuchumi katika kipindi kifupi kijacho kufuatia  matokeo ya kuuzwa kwake kwa  Mabalozi hao.

Mh. Membe amesema  Jamii ya Kimataifa kupitia ziara ya siku tatu ya Wanadiplomasia hao itafahamu uwepo wa Hitoria iliyopo Nchini Tanzania  hasa katika maeneo ya Ngorongoro, Serengeti pamoja na Zanzibar.

Akiwashukuru Wanadiplomasia hao kwa ujio wao hapa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema bado ana matumaini kwa Nchi rafiki kuendelea kufanyakazi kwa Ushirikiano wa pamoja na Tanzania.
Balozi seif amesema upanuzi wa Demokrasia  ndani ya Tanzania na Zanzibar kwa jumla umepelekea Jamii za Kimataifa kuunga mkono harakati za Maendeleo ya Taifa hili.

Mabalozi hao wa kigeni pamoja na wawakilishi wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa walikuwa katika ziara ya siku tatu kutembelea Sehemu za Kihistoria , uchumi pamoja na maeneo ya kumbu kumbu kuunga mkono maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amepokea mchango  kutoka kwa Ushirika wa kuongoza Magari ya Abiria wa Wilaya ya Kaskazini “A” kwa ajili ya Mfuko wa Maafa Zanzibar.
Katibu wa Ushirika huo Bwana Idrisa haji makame  amesema wao kama washirika wa wananchi waliopatwa na msiba kufuatia  ajali ya meli ya M.V Spice mwezi hivi karibuni wameguswa na maafa hayo.

Balozi Seif  ameushukuru Uongozi wa ushirika huo kwa ukaribu wao wa  kuwa pamoja na jamii katika msiba huo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
11/10/2011.

No comments:

Post a Comment