Na Anna Nkinda – Maelezo, Tarime
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ameitaka jamii nchini kutowaoza watoto wa kike wakiwa masomoni kwani ng’ombe wanaolipwa wazazi kama mahali hawana faida ukilinganisha na elimu ambayo angeipata mtoto huyo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliyasema hayo jana wakati akiongea na wakazi wa wilaya ya Tarime mkoani mara kwenye sherehe za kilele za wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru yaliyofanyika wilayani humo.
Alisema kuwa ni jambo la muhimu kwa wazazi na jamii kuwaruhusu na kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanasoma na hawakatishi masomo yao kwa kuwaoza au kupata ujauzito jambo ambalo linawafanya wanafunzi hao kutotimiza ndoto zao kwa kuwaharibia maisha yao kwani ukimuendeleza mtoto wa kike ni sawa na kuiendeleza jamii nzima.
Mama Kikwete alisema, “ Hivi sasa kuna tatizo kubwa la watoto wa kike kukatiza masomo baada ya kupata ujauzito na jambo la kusikitisha ni jinsi mzazi anavyoshirikiana na kijana aliyempa ujamzito binti yake kuharibu ushahidi na hivyo kufanya sheria kutochukua mkondo wake kwa kufanya hivyo mnasababisha watoto wasiwe waoga wa kufanya mapenzi kabla ya wakati na tazizo la mimba za utotoni kuwa sugu”.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka wanaume kuwasaidia wake zao kazi mbalimbali wanazozifanya hasa katika ulezi wa familia kwani ulezi wa mtoto ni wa wazazi wote wawili na jamii nzima inayowazunguka .
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo John Henjewele alisema kuwa pamoja na jitihada za halmashauri kuhakikisha watoto wanapata haki za msingi katika sekta ya elimu bado kuna tatizo kubwa la mimba mashuleni na ndoa za utotoni.
Alisema kuwa tangu mwaka 2008 hadi 2011 wanafunzi 46 wamepata ujauzito kati ya hao 33 ni wanafunzi washule za Sekondari na 13 ni wa shule za Msingi.
“Tatizo hili linasababishwa kwa kiasi kikubwa na mila na desturi potofu zinazoshawishi kufanyika kwa matendo hayo katika umri mdogo. Aidha uchukuaji wa hatua za kisheria unakatizwa na usiri uliopo kwa wananchi, hasa wazazi kuogopa au kukataa kuwafichua wahalifu”, alisema Henjewele.
Mama Kikwete alikuwa mkoani Mara kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na kilele cha wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambayo kilele chake kilifanyika jana katika wilaya ya Tarime.
No comments:
Post a Comment