MKOA WA KUSINI PEMBA 11/10/2011.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya kuwa na “sera ya mikopo” ambayo itawasaidia wafugaji, wavuvi na wakulima kupatiwa mikopo ili waweze kuendeleza miradi wanayoianzisha.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika ukumbi wa ZSSF ChakeChake alipokuwa akito majumuisho ya ziara yake ya siku mbili kisiwani Pemba kutembelea shughuli za Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Amesema wananchi wengi wamehamasika kuanzisha miradi ya mifugo na uvuvi, lakini wanakabiliwa na tatizo la mitaji, jambo ambalo linarejesha nyuma juhudi zao.
Amesema iwapo kutakuwa na utaratibu wa kupatiwa mikopo kwa wajasiriamali hao kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambao wengi wao hawana cha kufanya baada ya kumaliza masomo.
Amefahamisha kuwa miradi ya aina hiyo ni “mkombozi’ kwa wananchi, kwani inaweza kutoa ajira kwa watu wengi zaidi kwa wakati mmoja.
Maalim Seif amebainisha changamoto nyengine inayolikabili taifa katika sekta ya Mifugo na Uvuvi kuwa ni upatikanaji wa vyombo vya kuhifadhia bidhaa zitokanazo na sekta hizo zikiwemo samaki na mazima.
“Naiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi ifikirie ni kwa namna gani itaweza kuwasaidia wafugaji na wavuvi kuhifadhi bidhaa zao zisiharibike”, alisema Maalim Seif baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wafugaji na wavuvi aliokutana nao.
Aidha Makamu wa kwanza wa Rais ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutumia wataalamu wake kusukuma mbele maendeleo ya sekta hizo ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa mbegu za samaki kwa ajili ya wafugaji pamoja na kutafuta njia za kupunguza gharama za pembejeo zao zikiwemo chakula cha kuku na madawa.
Kwa upande mwengine Maalim Seif ameelezea umuhimu wa kutolewa elimu kwa wajasiriamali ili waweze kufanya shughuli zao kwa uhakika, na kuwataka wataalamu wa sekta hizo kuwa karibu nao ili waweze kuwasaidia pale wanapokwama.
Pia Makamu wa kwanza wa Rais ametaka elimu ya kutosha itolewe kwa wavuvi ili iwawezeshe kukabiliana na changamoto za uvuvi wa bahari kuu zikiwemo sheria za kimataifa na mawasiliano ya uhakika.
Vile vile Maalim Seif amesema bado serikali ina jukumu la kujipanga kuhakikisha kuwa miradi inayoanzishwa na wafadhili inaendelezwa baada ya kuondoka kwao, akitoa mfano wa shamba la ufugaji wa ng’ombe chamanangwe ambalo limepoteza hadhi yake baada ya kuondoka kwa wafadhili wa shamba hilo.
Hata hivyo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Said Ali Mbarouk amemuhakikishia Makamu wa kwanza wa Rais kuwa shamba hilo litafufuliwa na kuimarishwa katika kipindi kifupi kijacho.
Mapema Maalim Seif alitembelea maeneo mbali mbali ya uvuvi na ufugaji kuangalia maendeleo ya miradi iliyoanzishwa na wananchi ukiwemo mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa unaosimamiwa na Bi Khadija Said Mohd katika eneo la Kisiwani Kwa Binti Abeid.
Katika mazungumzo yake Maalim Seif amesifu juhudi zinazochukuliwa na mfugaji huyo pekee mwanamke katika kujiendeleza kiuchumi na kuwasaidia watu wengine kuweza kujiajiri.
“ Ni kweli kabisa kuwa wanawake wakiwezeshwa wanaweza, lakini bila ya mikopo hawafiki pahali kwa sababu mitaji yao ni midogo”, alisema Maalim Seif akisisitiza haja ya kuwepo sera ya mikopo nchini.
Ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwasaidia wajasiriamali hao juu ya namna ya kuweza kuzisarifu bidhaa zao ili ziweze kuhifadhika na kupata bei zaidi, sambamba na kushirikiana na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko katika kuwatafutia masoko ya uhakika kwa bidhaa zao zikiwemo, siagi na mtindi.
Maeneo mengine aliyoyatembelea ni kikundi cha wavuvi Mbuyuni Mkoani, Mradi wa ufugaji wa kuku unaoendeshwa na mayatima huko mbuguwani mkoani, maabara ya mifugo na maendeleo ya mradi wa CLES Machomanne, pamoja na kuzungumza na wajumbe wa kamati tendaji ya uvuvi na hifadhi ya mkondo wa Pemba huko Wesha.
Hassan Hamad (OMKR).
No comments:
Post a Comment