Friday, October 28, 2011

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI ANAONDOKA LEO KUELEKEA MAREKANI KIKAZI KWA SIKU KUMI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka  Nchini leo kwa safari ya Kikazi ya siku kumi  Nchini Marekani.  

Balozi  Seif aliyepata mualiko kutoka kwa shirika la uwekezaji vitega uchumi Afrika la Nchini Marekani anauongoza Ujumbe wa  Viongozi Sita  wa Kiserikali akiwemo Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi. 

Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  inalenga   Zanzibar kujitangaza zaidi Nchini Marekani katika Uwekezaji kwenye maeneo yaliyomo ndani ya Sekta za  Utalii, Biashara, Elimu, Kilimo, Afya, Miundo Mbinu pamoja  na Mazingira.

Viongozi anaofuatana nao katika Ziara hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha ,Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mh. Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Fatma Alhabib Fereji na Naibu Waziri wa Afya Dr. Sira Ubwa Mamboya.

Wengine ni Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Mh. Salmin Awadh Salmin, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Nd. Julian Raphael, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis Nassor wakiwemo pia  baadhi ya Wafanya biashara.

Balozi Seif na Ujumbe wake ataanza Ziara yake kwa kukutana na Uongozi wa Taasisi ya Biashara na Maendeleo { USTDA } pamoja na Mwakilishi wa  Taasisi ya Biashara na Vitega Uchumi inayosimamia Sera ya Biashara { USTR }.

Pia atakutana na Uongozi wa Shirika la Uwekezaji Vitega Uchumi
{ OPIG } linalofadhili Miradi ya Biashara ambapo siku inayofuata  atakaguwa Bandari ya  kwanza kwa upokeaji kwa wingi Bidhaa kutoka nje  ya Maarekani ya Houston kwenye Ghuba ya Mexico pamoja na kukutana na Washirika wa masuala ya Biashara Mjini Houston.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake ataendelea na ziara yake katika Mji wa Florida kwa kukitembelea Chuo Kikuu cha Kilimo na Ufundi cha Florida { FAMU }.

Balozi Seif anatarajiwa kuondoka Washington Nchini Marekani Tarehe 6 Oktoba 2011 na kurejea nyumbani akiuacha Ujumbe wake kuendelea na ziara ya siku tatu ya kukutana na Viongozi wa Taasisi mbali mbali za Uwekezaji Nchini humo ukiwemo Uongozi wa Benki Mashuhuri Duniani ya Exim Bank.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/10/2011.

No comments:

Post a Comment