Monday, October 24, 2011

WAGONJWA WA MOYO 611 KATI YA 1000 KWENDA INDIA KUFANYIWA MATIBABU YA MOYO

Na Fatma Mzee-Maelezo Zanzibar 24/10/2011

Wagonjwa wa Moyo 611 kati ya 1000 wanatarajiwa kuondoka Zanzibar kwenda nchini India kufanyiwa matibabu ya moyo ambapo kati ya wagonjwa hao wengi wao ni watoto wenye umri chini ya mika kumi na mbili.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Omar Abdalla Ali wakati alipokuwa akimkaribisha Hoyce Temu ambae aliwahi kuwa Mrembo wa Tanzani mwaka 1999 kwa lengo la kuwaona wagonjwa hao ili aweze kuwashawishi watu wenye uwezo kusaidia matibabu ya wagonjwa hao.

Katibu huyo alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali walifanikiwa kuwapeleka wagonjwa 662 nchini Izraeli na wagonjwa 125 kupelekwa India kwa matibabu ya Ugonjwa wa Moyo katika miaka iliyopita.

Aidha aliwataka wadau mbalimbali wenye uwezo kuzidi kulitilia mkazo suala la kuchangi matibabu kwa watu wenye mahitaji ili kuisaidia Serikali katika kukabiliana na matatizo ya kiafya kwa wananchi wake.

Kwa upande wake Mrembo huyo wa Tanzania Hoyce Temu aliwaahidi wazazi wa watoto wenye matatizo ya moyo kuwa atatumia nguvu zake zote kwenda kuwashawishi watu wenye uwezo ili kuhakikisha wanachangia huduma za matibabu kwa wagonjwa hao.

Aidha Hoyce Temu alisema kuwa atarudi Zanzibar baada ya Wiki Moja ili kuleta mchango wowote atakaofanikiwa kuukusanya kutoka kwa wadau mbalimbali ili uweze kusaidia katika Safari ya hiyo ya India.

Amesema atakapo rudi Zanzibar ataanza na safari ya watoto sita ambao watakuwa na hali mbaya zaidi huku wengine wakisubiri kupatikana msaada ili nao wapelekwe huko India.


Aidha Mrembo huyo aliaahidi pia kushirikiana na Madaktari wa Mmanazi Mmoja na wazazi hao ili kuhakikisha tatizo hilo linaweza kupunguwa kwa kiasi kikubwa.

Amewataka Wazanzibari wenye uwezo kulichukulia umuhimu suala hilo ili kuweza kusaidia wanyonge na watu watu wasikuwa na uwezo wa kuwapeleka watoto wao matibabuni.

Nao baadhi ya wazazi wa watoto hao walimshukuru Hoyce Temu kwa ahadi zake na kuwaomba watu wenye uwezo hasa kwa kwa upande wa Zanzibar kusaidia watoto hao kwa hali na mali kwani fungu lao kubwa litabaki kuwa kwa Mungu.

No comments:

Post a Comment