Monday, October 24, 2011

MAALIM SEIF ASEMA KUNA HAJA KWA WATENDAJI WA SERIKARI KUTEKELEZA KWA HARAKA MAAMUZI YA VIKAO

Maalim Seif akimueleza mwenyekiti wa   Baraza la mpango wa Afrika wa kijitathmini katika utawala bora (APRM) nchini Tanzania Bw. John Shibuda, wakati ujumbe wa Taasisi hiyo ulipofika OMKR Migombani kutoa tathmini ya utafiti wao.
Maalim Seif akisikiliza tathmini ya ripoti ya APRM kuhusu Utawala Bora Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar (Picha: Salmin Said OMKR).


Na: Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuna haja kwa watendaji wa serikali kutekeleza kwa haraka maamuzi yanayofikiwa kwenye vikao vya juu vya kutatua kero za Muungano ili kuondoa malalamiko kwa wananchi.
Maalim Seif amesema hayo leo huko ofisini kwake migombani alipokutana na wajumbe wa Baraza la mpango wa Afrika wa kijitathmini katika utawala bora (APRM) nchini Tanzania waliofika kuwasilisha tathmini  ya utafiti wao.
Makamu wa kwanza wa Rais amesema serikali imeunda kamati ya kutatua kero za Muungano ambayo kwa Zanzibar inaongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, na Tanzania Bara inaongozwa na Waziri Mkuu kwa nia njema, hivyo watendaji hawanabudi kufanikisha azma hiyo kwa kutekeleza yale yanayotolewa maamuzi.
Makamu wa kwanza wa Rais amesema miongoni mwa mambo yaliyofikiwa maamuzi ni pamoja na suala la wafanyabiashara kutozwa kodi katika bandari wanayofikisha bidhaa zao mara ya kwanza, lakini hadi sasa kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara hasa wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.
Amefahamisha kuwa tabia kama hiyo haina budi kukomeshwa, kwa vile inarejesha nyuma juhudi za wananchi kujiendeleza kiuchumi.
Aidha Maalim Seif ameelezea kuwepo utitiri wa taasisi za kukusanya kodi nchini na kutaka kuangaliwa uwezekano wa kupunguzwa kwa taasisi hizo.
katika tathmini yao wajumbe hao wamebainisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na serikali yao juu ya kero za Muungano.
Akizungumzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Mwenyekiti wa taasisi hiyo John Shibuda amesema serikali hiyo imeleta mafanikio makubwa na ni mfano wa kuigwa na Tanzania na nchi nyengine barani Afrika hasa katika nchi ambazo zimekuwa zikikumbwa na migogoro ya kisiasa.
Bw. Shibuda Amesema kuna haja ya ufuatiliaji wa karibu wa utendaji wa serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar, ili uweze kuwa endelevu na kuwasiliana na uongozi wa bunge ili kumuomba Makamu wa kwanza wa Rais kutoa taaluma na uzoefu wake juu ya Serikali hiyo kwa wabunge.
“Wabunge tunahitaji sana kujifunza uzoefu na mafanikio ya serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar”, amesema kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi.
Maalim Seif amesema mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa yamepatikana kutokana na nia njema ya waanzilishi wa maridhiano na wananchi wa Zanzibar kumaliza migogoro na kujiletea maendeleo.
Akizungumzia uchumi na maendeleo Makamu wa kwanza wa Rais amesema bado Zanzibar iko nyuma katika Sekta ya Viwanda na kwamba inahitaji kujiendeleza ili kuweza kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Mbali na Viwanda, Maalim Seif amesema serikali ina nia thabiti ya kuliendeleza zao la karafuu, ili katika kipindi cha miaka kumi ijayo zao hilo liweze kurejeshewa hadhi yake kama ilivyokuwa hap kabla.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amesema serikali inaendelea na mkakati wake wa kuimarisha miundo mbinu ya usafiri ili kuwawezesha wafanya biashara na wawekezaji kufanya shughuli zao bila usumbufu.
“Tatizo letu kwa sasa ni usafiri wa baharini na angani, lakini kwenye barabara tumepiga hatua kubwa. Namshukuru sana Rais mstaafu Dkt Karume kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuimarisha barabara”, amesema Maalim Seif.
Mapema akiwasilisha ripoti ya tathmini ya utafiti wao kuhusiana na utawala bora, Katibu mtendaji wa Taasisi hiyo ya The African Peer Review Machanism (APRM Tanzania) bibi Rehema Twalib lengo la tathmini hiyo ni kujenga fikra endelevu kwa maslahi ya nchi.
Nae mjumbe wa taasisi hiyo Bw. Salim Said amelalamikia uwakilishi mdogo wa wajumbe wa Zanzibar kwenye Taasisi hiyo ambapo kati ya wajumbe 20 Zanzibar ina wajumbe wawili pekee.
Jumla ya nchi 30 za Afrika zinashiriki katika mchakato huo huo wa kujitathmini ambapo kwa kuanzia kila nchi hujitathmini yenyewe na baadae wataalamu wa mpango huo kutembelea kila nchi ili kutoa maoni yao kuhisiana na tathmini zinazotolewa.

No comments:

Post a Comment