Friday, October 14, 2011

TAARIFA YA KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI JUU YA AJALI YA MELI

Jengo la Baraza la Wawakilishi Zanzibar

Na Khadija Khamis - Maelezo Zanzibar 

Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa juuya tukio la kuzama kwa meli ya  Mv Spice Islanders-1, imemtaka Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad kujiuzulu kwa hiyari yake kutokana na uzembe wa kutosimamia majukumu yake aliyopewa na Serikali .

Akitoa taarifa juu ya Ajali ya Meli hiyo mbele ya Baraza la Wawakilishi leo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hamza Hassan alieleza kuwa kutokana na uzembe huo uliofanywa na Wizara yake imeonyesha wazi kuwa Waziri huyo ameshidwa kusimamia ipasavyo majukumu yake aliyopewa na Rais.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza Mamlaka ya Usafiri Baharini, kuna kipengele kinachomtaka Waziri kuunda Tume ya Uchunguzi pale linapotokea janga kama hilo lakini Waziri huyo alishindwa kuunda tume .

Aidha Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Rais aliamua kuunda Tume wakati wajibu huo ulikuwa ufanywe na Waziri huyo mapema.

Kamati hiyo ilieleza kuwa inaamini kwamba kujiuzulu kwa Waziri wa miundo mbinu na mawasiliano kutapanua wigo wa demkrasia pamoja na uwajibikaji.

Kamati hiyo ilieleza kuwa kumetokea uzembe mkubwa kwa Nahodha wa meli hiyo kwa kushindwa kutoa taarifa mapema wakati meli ilipoanza kuingia  maji hadi hapo abiria wenyewe kuanza kupiga simu wakiwa juu ya meli na inaanaaminika kwamba kama Nahodha angelitoa taarifa mapema basi abiria wengi sana wangeliokolewa wakiwa hai .

Mwenyekiti huyo alieleza kwamba kwa vile tukio hilo lilitokea usiku  kama wangelipiga fataki kurusha angani ingelisaidia kutoa ishara kwa waokoaji kuona chombo kilipokuwa na kuweza kutoa msaada.

Kamati imeeleza kuwa kwa mujibu wa taratibu za meli yoyote ni lazima ziwe na vifaa vya kuokolea na mawasiliano ikiwemo fataki za kupiga angani pale inapotokea janga kama hilo.

Meli ya Mv  Spice Islanders-1,ilitengezwa mwaka 1974 na kufanyiwa marekebisho makubwa nchini Ugiriki mwaka 200I.

Meli hiyo yenye urefu wa mita 58,15 na upana wa mita 11.4   ilinunuliwa na Visiwani Shipping Company mwaka 2007 na kupatiwa usajili 2007 baada ya kufanyiwa ukaguzi kwa mujibu wa sheria na kuruhusiwa kuchukua abiria 600 na mizigo tani500.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIIBAR

No comments:

Post a Comment