Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Perth, Australia, jioni ya leo, Jumanne, Oktoba 25, 2011, kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Madola (Commonwealth Heads of Government Meeting – CHOGM) mwaka huu.
Rais Kikwete akiongozana na Mama Salma Kikwete amewasili mjini Perth tayari kujiunga na viongozi wenzake wa nchi za Jumuia ya Madola kwa ajili ya mkutano uliopangwa kuanza Ijumaa, Oktoba 28, 2011, katika ukumbi wa Riverside Theatre.
Kama ilivyo kawaida, Mkutano huo wa CHOGM ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, umetanguliwa na Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za Nje za Jumuia ya Madola na wakati CHOGM inaendelea itakuwepo mikutano mingine ikiwa ni pamoja na Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Vijana, Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Biashara na Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Wananchi .
Hii itakuwa mara ya tatu kwa Rais Kikwete kuhudhuria Mkutano wa CHOGM tokea ashike madaraka ya kuongozwa Tanzania miaka sita iliyopita. Alishiriki mikutano ya CHOGM iliyofanyika mjini Kampala, Uganda, mwaka 2007, na mjini Port of Spain, Trinidad na Tobago, mwaka 2009.
Mbali na kuhudhuria Mkutano wa CHOGM, Rais Kikwete atatumia nafasi ya Mkutano huo kukutana na viongozi mbali mbali wa nchi na mashirika ya kimataifa ya sekta za umma na sekta binafsi.
Miongoni mwa shughuli zake za kwanza kesho, Rais Kikwete anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Jumuia ya Watanzania wanaoishi katika eneo la Australia Magharibi.
Keshokutwa, Rais Kikwete atakuwa mzungumzaji katika mdahalo kuhusu jinsi ya kuwawezesha akinamama ili waweze kuongoza – Empowering Women to Lead- ulioandaliwa na Mheshimiwa Julia Gillard, Waziri Mkuu wa Australia na mwenyeji wa CHOGM mwaka huu baada ya ameshikiri katika halfa kuhusu suala hilo hilo itakayoandaliwa na Mheshimiwa Quetin Bryce AC, Ganava Mkuu wa Australia (The Commonwealth of Australia).
Keshokutwa hiyo hiyo, Rais Kikwete pia atakuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Biashara ambako atatoa hotuba maalum yenye mada: “Africa: Creating a New Economic Power for the 21st Century”. Siku hiyo hiyo, Rais Kikwete atakuwa mwenyekiti wa mkutano kuhusu suala la madini kati ya Tanzania na Australia wa “Tanzania-Australia Mining Roundtable” ambao utahudhuriwa na baadhi ya wafanyabiashara.
Miongoni mwa mambo makubwa yatayojadiliwa kwenye Mkutano wa CHOGM mwaka huu ni pamoja na viongozi wa nchi wanachama wa Jumuia kuangalia jinsi ya kuimarisha uwezo wa Jumuia katika kuunga mkono demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora miongoni mwa nchi wanachama waa Jumuia hiyo.
Mkutano huo pia utajadili jinsi ya nchi wanachama wanavyoweza kukabiliana na changamoto za sasa za kimataifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uchumi endelevu, jinsi ya kuondokana na matatizo za sasa ya kiuchumi duniani na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano pia utajadili changamoto za usalama wa chakula duniani, maendeleo endelevu na menejimenti ya maliasili.
No comments:
Post a Comment