Monday, October 10, 2011

SERIKALI ITAENDELEA KUFUATILIA MIJADALA KUHUSU FAIDA NA HASARA ZA ADHABU YA KIFO ILI KUPIMA NA KUTAZAMA KAMA IPO HAJA AU LAA YA ADHABU HIYO

Serikali itaendelea kufuatilia kwa makini mijadala kuhusu faida na hasara za adhabu ya kifo ili kupima na kutazama kama ipo haja au laa ya kuondosha adhabu ya Kifo ambayo bado sheria hiyo   haijafutwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo kwenye Maadhimisho ya Siku ya kupinga Adhabu ya Kifo Duniani zilizofanyika katika Ukuimbi wa Mikutano wa Eacrotanal Mjini Zanzibar.

Maadhimisho hayo yameambatana na Uzinduzi wa  Vitabu Viwili 
Vinavyoitwa Adhabu ya Kifo katika Sheria za Kiislamu kilichotungwa na Mwachuoni Maarufu hapa Zanzaibar Dr. Muhyiddin Ahmad Khamis.

Kitabu Chengine kimetungwa kwa Lugha ya Kiingereza kinachoitwa Zanzibar: The Development of the Consitution kilichokusanya maandiko ya Wataalamu wa Sheria akina Profesa Chris Maina Peter, Dr. Sengodo Mvungi, Bwana Ali Uki na Bwana Yahya Khamis Hamad.

Akizungumza katika Maadhimisho hayo Balozi Seif Ali Iddi amesema kwa vile Sheria ya Kifo bado haijafutwa Nchini, Hivyo ipo haja kwa Jamii  kushiriki katika mijadala iliyopo ya masuala hayo badala ya kuwaachia wasomi pekee.
Akizungumzia Fani ya Uandishi wa Vitabu Balozi Seif amesema eneo hilo kwa muda mrefu linaonekana kuchechemea .
Amewaomba Wenye Uwezo wa Kuandika wafanye hivyo badala ya Fani hiyo kuwaachia Wageni pekee.

Mapema Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakari amesema hakuna hukumu hata moja ya kifo iliyotekelezwa hapa Zanzibar licha ya Mahkama Kuu kutoa Maamuzi tokea mwaka 1964.

Maadhimisho hayo yameambatana na Mijadala na kuwashirikisha Wataalamu wa Fani ya Sheria, Wasomi pamoja na Washirika wa Fani hiyo.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment