Friday, October 7, 2011

MAALIM SEIF ASIFU HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA HOSPITALI YA MADRASA INSTITUTE OF ORTHOPEDIC AND TRAUMA

Meneja wa masoko ya nje wa Hospitali ya Madrasa Institute Orthopedic and Trauma (MIOT) ya India GALAL AHMED DAWOOD akimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad juu ya  huduma zinazotolewa na hospitali, wakati ujumbe wa hospitali hiyo ulipofanya mazungumzo ya Maalim Seif Ofisni kwake Migombani.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Dr. AJII PAI ambaye ni mtaalmu wa upasuaji kutoka hospitali ya MIOT ya India alipofika OMKR na madaktari wenzake kutoka MIOT kuzungumza nae juu ya huduma mbali mbali zinazotolewa na hospitali hiyo.
 
Na: Hassan Hamad (OMKR)
 
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesifu hatua  zinazochukuliwa na hospitali ya Madrasa Institute of Orthopedic and Trauma (MIOT) ya Chennai, India za kuleta huduma zake Zanzibar na kuwapunguzia gharama kubwa wananchi kuzifuata huduma hizo nje ya nchi.

Maalim Seif ameeleza hayo huko ofisini kwake migombani mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa madaktari kutoka hospitali hiyo.

Amesema wataalamu wa afya kutoka nje wanahitajika sana Zanzibar kwa sababu kuna wagonjwa wengi wanaotibiwa nje ya nchi lakini gharama za usafiri na matibabu ni kubwa.

Maalim Seif amesema Zanzibar kuna watoto wengi wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo, na kutakiwa kwenda matibabuni India, hivyo hatua za kutolewa huduma hizo Zanzibar ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Unguja na Pemba.

Kwa upande wake waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji ambaye alihudhuria kwenye mazungumzo hayo amesema Wizara hiyo itatoa mashirikiano yote kwa madaktari kutoka nje ya nchi ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi.

Amewashauri madaktari hao kuleta mashine na vifaa vya kisasa hapa Zanzibar kurahisisha matibabu kwa wananchi na kupunguza Idadi ya wananchi wanaopewa rufaa za matibabu nje ya nchi hasa nchini India.

Kiongozi wa madaktari hao Galal Ahmed Dawood amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Zanzibar katika kutoa huduma za afya, ambapo wagonjwa wapatao 200 tayari wamepatiwa matibabu katika hospitali ya MIOT huko Chennai, India.

Amesema nia ya kukutana na Makamu wa kwanza wa Rais ni kupongeza hali ya mashirikiano makubwa wanayopewa Zanzibar na kuomba yazidi kuimarishwa kwa leo la kuwasaidia wananchi wa Zanzibar kupata matibabu ya uhakika.

No comments:

Post a Comment