Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema umefika wakati kwa Jamii ya Waumini wa Dini ya Kiislamu kuongeza nguvu zao katika kujenga vituo vya amali na madrasa ndani ya Misikiti Mipya wanayoijenga kwa lengo la kuongeza ajira kwa Vijana.
Balozi Seif ametoa kauli hiyo wakati akiufungua Msikiti mpya wa Ijumaa uliopo Mtaa wa Miembeni Mjini chake chake Pemba hafla iliyoambatana na Sala ya Ijumaa iliyoshirikisha pia Jopo la Maulamaa na Baadhi ya Viongozi wa Taasisi za Dini ya Kiislamu kutoka Kisiwani Unguja.
Amesema Serikali Kuu pamoja na juhudi zake za kuimaisha Uchumi wake bado inaendelea kukabiliwa na ongezeko kubwa la Vijana wasiokuwa na ajira.
Amesema hatua ya uwekezaji wa vianzio vya ajira ndani ya misikiti itapelekea Vijana waliowengi kuongezeka Misikitini na tatizo la ajira linalokabili Vijana hao litapungua.
Balozi Seif alisisitiza kwamba uzuri wa Msikiti ni utoaji wa huduma bora kwa Waumini. Hivyo ni vyema kwa Majengo hayo yakatumiwa na Waumini katika kujenga mshikamano.
“ Itakuwa ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kuona Waumini wanagombea Msikiti. Msikiti ni Pahala pekee pa kupiga vita ibilisi ”. Alisema Balozi Seif Ali Iddi.
Aliongeza kusema kwamba ni vyema kwa Waumini wakawajengea imani Wafadhili wanaofadhili ujenzi wa misikiti ili wafarajike katika kuendelea kutoa misada yao.
Akizungumzia suala la uadilifu na uaminifu ndani ya jamii Balozi Seif amesema vitendo hivyo hivi sasa vinatisha kiasi ambacho maisha ya Wananchi yataendelea kuwa magumu.
Amesema ni jambo la kawaida kwa sasa kuona baadhi ya wazazi kupendelea watoto wao wafanye kazi katika Taasisi zenye Mapato makubwa kwa Tamaa ya Utajiri wa Haraka.
“ Maeneo hayo ya Mapato makubwa mara nyingi yametawaliwa na tamaa ya utajiri unaotaka kujengwa kwa vitendo vya rushwa na wizi ”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba ukosefu wa uaminifu na uadilifu katika jamii unarejesha nyuma Maendeleo ya Nchi na wakati mwengine husababisha Maafa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameahidi kusaidia maendeleo ya Skuli ya Maandalizi iliyoanzishwa katika Msikiti huo.
Mapema wakisoma Risala yao Waumini wa Msikiti huo wa Ijumaa wa Mtaa wa Miembeni Chake Chake wamewaomba watu wenye uwezo kuendelea kutumia mali zao kwa kuongeza nguvu katika kuimarisha miradi ya kiuchumi ndani ya Uislamu.
Wamesema hatua hiyo itajenga nguvu kwa waumini kutekeleza vyema Dini yao sambamba na kujipatia Kipato chao kwa njia ya Halali.
Na: Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makmu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
7/10/2011.
No comments:
Post a Comment