Tuesday, October 11, 2011

DR. SHEIN AMESEMA KUWA NA MAENDELEO YOYOTE YA NCHI HUTEGEMEA ELIMU PAMOJA NA KUWEPO WATU WALIOELIMIKA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa maendeleo yoyote ya nchi yanategemea elimu pamoja na kuwepo watu walioelimika.
 
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa akitoa nasaha zake na pongezi kwa  wanafunzi waliopata Daraja la Kwanza katika mtihani wa Kidato cha Nne na Sita mwaka 2010/2011 katika skuli za Zanzibar, ambapo pia, Dk. Shein alikula nao chakula maalum alichowaandalia katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar..
 
Katika maelezo yake Dk. Shein  alisema kuwa kwa kutambua umuhimu huo wa elimu ndio maana Serikali anayoiongoza ikaweka mkazo mkubwa katika utanuzi wa elimu katika ngazi zote ingwa kwa hivi sasa mkazo mkubwa umewekwa kwa elimu ya Sekondari na Vyuo Vikuu.
 
Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo imepelekea ongezeko kubwa la wanafunzi waliomaliza masomo ya Kidatu cha Nnne na Kdato cha Sita na wenye sifa za kwenda Vyuo Vikuu.
 
Alisema kuwa kwa mwaka huu jumla ya wanafunzi 1603 wameomba mikopo ya kusoma katika vyuo vya elimu ya juu katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar hatua ambayo inadhihirisha wazi kuwa vijana wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani yao.
 
Dk. Shein alisema kuwa Serikali inatumia fedha nyingi sana kwa kuekeza katika ujenzi wa skuli mpya 21 za kisasa za Sekondari zinazojengwa  Unguja na Pemba, ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo  Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) huko Tunguu pamoja na ujenzi wa Kampasi ya Chuo cha Ualimu cha Benjamin Willium Mkapa, huko Mchanga Mdogo Pemba na .
 
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 70  katika miradi hiyo na kusisitiza kuwa Serikali imeamua kufanya hivyo kutokana na manufaa yatakayopatikana katika uwekezaji huo.
 
Dk. Shein aliwanasihi wanafunzi hao kuelewa na kuthamini juhudi zinazochukuliwa na serikali yao katika kusambaza huduma za elimu na kuwataka kusoma kwa bidii na kwa wale watakaosoma nje ya nchi baada ya kumaliza masomo yao warudi nyumbani ili waje kuitumikia nchi yao na watu wao.
 
Dk. Shein aliwataka wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao pamoja na kuwashauri waalimu kuendelea kuwasomesha vijana kwa juhudi kubwa kwani taifa linawategemea wao.
 
Dk. Shein pia, aliwaeleza wanafunzi hao tatizo la kuzagaa kwa dawa za kuelvya na utumiaji wake hapa Zanzibar na nchi zote duniani na kueleza kuwa kufaulu kwao wao na wenziwao waliokuwa hakupata nafazi ya kufika hapo ni ishara nzuri kuwa wamenusurika na tatizo hilo na kuwataka washirikiane na vijana wenzao kupiga vita dawa za kulevya ambazo madhara yake ni makubwa.
 
Kutokana na umuhimu wa waalimu nchini Dk. Shein alieleza kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea katika kuyanyanyua maslahi yao  ili waweze kufanya kazi kwa utulivu zaidi na kuendelea kuipenda kazi yao.
 
“Ni jukumu letu serikali kulisimamia hili.. tutaanza Octoba hii, tuliahidi na nasema kuwa Octoba hii mambo yatabadilika na Waziri wangu  anayeshughulikia Fedha, amenihakikishia kuwa mambo poa kabisa”,alisema Dk. Shein huku waalimu na wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo wakiangusha kicheko kwa furaha.
 
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wanafunzi hao kuwa anaelwa kuwepo kwa uhaba wa madawati, vifaa vya sayansi, uhaba wa madarasa na waalimu wa kufundisha masomo ya Sayansi na kueleza azma ya Serikali anayoiongoza kuondosha changamoto hizo zote zinazoikabili sekta ya elimu nchini hasa vifaa vya maabara.
 
Wakati huo huo pia, Dk. Shein alitoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi pamoja na kuahidi kuendeleza utaratibu wa kuwaalika Ikulu wanafunzi wote waliofaulu Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Sita na Nne katika daraja la Kwanza.
 
 Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ali Mhe. Ramadhan Abdala Shaaban alisema kuwa wanafunzi waliofaulu na kutunukiwa cheti cha daraja la Kwanza ni 116, kati yao wanafunzi 92 ni Kidato cha nne na wanafunzi 24 ni Kidato cha Sita ambao wanatoka katika skuli za Sekondari 26 za Unguja na Pemba zikiwemo skuli binafsi ambao nao walijumuika katika hafla hiyo.
 
Waziri Shaaban alisema kuwa Wizara yake inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa skuli zote za Sekondari zinatoa elimu bora ya kiwango cha juu na kueleza kuwa tayari skuli hizo zimepatiwa vitabu vya kufundishia vya kutosha kwa waalimu wote.
 
Nao wanafunzi hao wakisoma risala yao kwa Rais Dk. Shein walieleza kufurahishwa kwao na muwaliko huo walioupata wa kufika Ikulu na kupongezwa na Rais na kutoa pongezi kwa niaba ya wanafunzi wote kwa ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu wa mwezi Octoba mwaka jana na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
 
Walieleza kuwa wanaamini chini ya uongozi wa Dk. Shein watajengewa mazingira mazuri ya kujifunza yakiwemo yale ya kupatiwa nafasi nyingi za kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwani mwaliko huo ni changamoto na motisha ya kuendelea na elimu yao ya juu.
 
Aidha, wanafunzi hao waliahidi kuendelea kuwa watiifu kwa serikali kwa muda wote wa maisha yao pamoja na kuzitumia vyema fursa za masomo na za udhamini wa masomo wanazopewa na serikali yao na kutumia elimu watakayoipata kwa faida ya nchi yao.
 
 Rajab Mkasaba
 Zanzibar                                                                                               11.10.2011

No comments:

Post a Comment