Friday, October 21, 2011

KAMISHNA WA UTALII, UTAMADUNI NA MICHEZO AWATAKA WASANII KUONGEZA SANAA ZENYE UBORA

NA AZIZI SIMA-MAELEZO  PEMBA 21/10/2011

Kamishina wa Utalii, Utamaduni na Michezo Zanzibar  Hamad Bakari Mshindo amewataka wasanii nchini kutengenza Sanaa zenye ubora ilikuweza kuvutia watalii wanaokuja nchini pamoja na kupata soko la kuweza kuuza bidhaa zao.

Mshindo ameeleza hayo Gombani alipokuwa akizungumza na wasanii wa Pemba kwa lengo la kukumbusha wajibu wao katika kazi za sanaa za ufundi.

Amesema kuwa wageni wengi hupendelea sanaa za Kizanzibari lakini  baadhi ya sanaa nyengine hukosekana vionjo vya kizanzibari  katika usanifu wake na kupelekea bidhaa hizo kama mikoba, kofia  na mikeka kukosa soko kutokana na kukosekana kwa vionjo hivyo.

Amesema kuwa iko haja kwa wasanii kubadilika na kushirikiana katika kazi zao za usanii ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi vya ushirika hasa kwa vile Pemba ina wasanii wengi ambao wanahitaji soko na taaluma

Kamishina Mshindo amesema kuwa katika bajeti ijayo Kamisheni yake itawashirikisha wasanii katika kuandaa bajeti ili kuweza kujua mahitajio yao ambayo yatapaswa kutekelezwa kwa lengo la kujaribu kupunguza changamoto zinazo wakabili wasanii hao.

Pia amewataka wasanii hao kutengeneza sanaa kwa wingi kwa lengo la kuuza katika soko la ndani na nje ya nchi badala ya kutengeneza  sanaa kidogo ambazo haziwezi kupata soko kubwa.

No comments:

Post a Comment