Tuesday, October 25, 2011

MAALIM SEIF ASEMA SERIKALI INATOA UMUHIMU WA KIPEKEE KULINDA ARDHI YA VISIWA VYA UNGUJA NA PEMBA

Balozi wa Finland nchini Tanzania SINIKKA ANTILA akizungumza na Maalim Seif alipofika Ofisini kwake Migombani kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali hasa yanayohusu mazingira.
Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej akizungumza na Balozi wa Finland nchini Tanzania SINIKKA ANTILA Ofisini kwake Migombani. (Picha Salmin Said-OMKR)

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali inatoa umuhimu wa kipekee kuilinda ardhi na mazingira ya visiwa vya Unguja na Pemba yasiharibiwe na matendo ya binadamu na athari za majanga ya kimaumbile.

Maalim Seif ameeleza hay oleo alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Finland nchini Tanzania Bibi Sinikka Antila alipofanya mazungumzo nae huko Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.

Amesema miongoni mwa changamoto zinazotaka zipatiwe ufumbuzi wa haraka na serikali ni ongezeko la watu katika maeneo ya mijini, ukataji miti ovyo pamoja na baadhi ya wananchi kufanya ujenzi katika maeneo yasiyoruhusiwa yakiwemo ya kilimo na maeneo ya wazi.

Makamu wa kwanza wa Rais amesema juhudi kubwa zinachukuliwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi hasa kwa vile nchi za visiwa kama Zanzibar yenye ardhi ndogo, inaweza kukosa ardhi kwa matumizi ya mambo ya maendeleo na kijamii.

“Matumizi ya ardhi ni suala linalotuumiza vichwa sana, baadhi ya watu wana tabia ya kujenga kwenye maeneo yenye rutba yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo, maeneo ya wazi na tunakabiliana na tatizo la ukataji miti ovyo hata kwenye vyanzo vya maji”, amesema Maalim Seif Seif.

Pia Maalim Seif ameelezea mkakati wa kupanda miti katika maeneo yaliyoathiriwa na uchafuzi wa mazingira hasa katika kisiwa cha Pemba, ili kujikinga na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameanza kujitokeza.

Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania Bibi Sinikka Antila amesema nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika suala la uhifadhi wa mazingira.

Amesema mazingira ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, hivyo hayana budi kulindwa na kuhifadhiwa kwa nguvu zote ikiwa ni pamoja na kupanda miti.

“Nchini kwetu kuna kanuni isemayo, ‘kata mti mmoja panda miwili’”, alisema balozi Sinikka.

Finland ni miongoni mwa nchi zinazotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar hasa katika masuala ya mazingira ambapo kwa sasa inasimamia mradi mkubwa wa usimamizi wa ardhi na mazingira Zanzibar (SMOLE).

No comments:

Post a Comment