Na: Hassan Hamad (OMKR)
Makampuni yanayojishughulisha na ununuzi wa zao la Mwani nchini yametakiwa kujirekebisha na kutoa bei ya zao hilo kwa mujibu wa soko la dunia ili kuwawezesha wakulima kuongeza kipato chao kulingana na gharama za uzalishaji wanazotumia.
Akizungumza na wakulima wa mwani katika shehiya ya Kiuyu mbuyuni Wilaya ya Micheweni Pemba, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema iwapo makampuni hayo yatashindwa kufanya hivyo, Serikali inaweza kuingilia kati na kuliruhusu Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar ZSTC kununua zao hilo kwa maslahi ya wakulima na Taifa kwa jumla.
Amesema kazi ya uzalishaji wa mwani ni ngumu na kwamba bei ya sasa ya shilingi 400 kwa kilo hailingani na jasho la wakulima.
Amefahamisha kuwa zao la mwani limekuwa miongoni mwa mazao makuu ya biashara Zanzibar, hivyo linastahili kuendelezwa ili kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi na kuinua pato la taifa.
“Mazao ya mbata, usumba, pilipili hoho na mengineyo yaliyokuwa yakizalishwa zamani yote nafasi yake imechukuliwa na mwani”, alikumbusha Maalim Seif.
Amesisitiza kuwa nia ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuona kuwa wakulima wa mazao ya biashara wanapata asilimi 80 ya bei ya soko la dunia, na tayari imefanikiwa kwa zao la karafuu na inakusudia kufanya hivyo kwa zao la mwani.
Nae Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Said Ali Mbarouk amesema licha ya bei ya zao hilo kuwa ndogo lakini limewasaidia wakulima wa eneo hilo kubadilisha hali zao za maisha.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt KASSIM GHARIB JUMA ameahidi kuwasaidia wakulima hao kitaaluma ili waweze kuusarifu mwani kwa kutengeneza bidhaa nyengine zitokanazo na mwani zikiwemo sabuni, keki na vileja.
Jumla ya tani 12,500 za mwani zilizalishwa Zanzibar mwaka uliopita ambapo mwaka huu wa 2011 wanatarajia kuzalisha tani 14, 000.
Wakulima 2300 wanajishulisha na kilimo cha mwani katika shehiya ya Kiuyu-mbuyuni pekee, wengi wao wakiwa wanawake.
Katika ziara hiyo ya kutembelea Wizara ya Mifugo na Uvuvi kisiwani Pemba, Maalim Seif pia alitembelea vikundi vya ufugaji wa samaki Kangagani, Shamba la ng’ombe Chamanangwe, Ujenzi wa soko la samaki Tumbe na Ujenzi wa jingo la Idara ya uvuvi Pemba lililoko Weni-Wete.
Meneja wa shamba la ng’ombe Chamanangwe Bw. KOMBO SEIF KHAMIS amesema shamba hilo linalokusudiwa kuwa kituo cha utafiti Pemba, linakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo tatizo la maji kwa ajili ya mifugo, na kwamba iwapo litawezeshwa linaweza kuwanufaisha wafugaji wengi zaidi wa kisiwa cha Pemba.
No comments:
Post a Comment