Sunday, October 9, 2011

DW: MAITI YA WANGARI MAATHAI IMECHOMWA LEO KAMA ALIVYOAGIZA

Profesa Wangari Maathai wakati wa uhai wake
 
Shughuli ya kumuaga Marehemu Prof. Wangari Maathai imefanywa leo katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi kabla mwili wake kuteketezwa katika makaburi ya Kariokor.
Wananchi wa Kenya leo wanamuaga mwanamke wa kwanza wa Afrika kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel katika mazishi ya yanayojumuisha sala, pongezi na upandaji wa miti. 

Mamia ya Wakenya akiwemo Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga wamekusanyika katika uwanja mashuhuri wa Uhuru katika mji mkuu wa Nairobi kuhudhuria sala za kumuombea Wangari Maathai. Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel ambaye anajulikana sana kwa jina la Mama Mti wa Afrika alianzisha shirika la Green Belt Movement lililopanda miti milioni 30 nchini kote Kenya.

Maathai alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel hapo mwaka 2004. Alitambuliwa kwa kazi yake ya kuhifadhi mazingira na kutetea haki za wanawake mambo ambayo yalimfanya apambane na serikali ya ukandamizaji ya Rais wa zamani Daniel arap Moi.

Maathai amefariki mwezi uliopita kutokana na kuuguwa saratani. Alikuwa na umri wa miaka 71.

Mwandishi: Mohammed Dahman
Mhariri: Josephat Charo

No comments:

Post a Comment