Thursday, November 3, 2011

ZANZIBAR YASHAURIWA KULITUMIA VEMA SOKO LA AFRIKA MASHARIKI KUKUZA UCHUMI

Zanzibar imeshauriwa kulitumia vyema soko la Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Mashariki kwa lengo la kukuza uchumi wake na kuondokana na kutegemea zao moja la karafuu kama mhimili wa Taifa.

Ushauri huo umetolewa na Mkamu wa Rais wa Shirika la uwekezaji Vitega Uchumi la Kimataifa Nchini Marekani  { OPIC } Bibi Mimi  Alemahou wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  hapo Makao Makuu ya Shirika hilo Mjini Washington DC Nchini Marekani.

Bibi Mimi alimueleza Balozi Seif  na ujumbe wake ulioko nchini Marekani kwa ziara ya Kikazi ya kuitangaza Zanzibar kwa wekezaji kuwekeza Zanzibar kwamba Shirika hilo tayari limeshaandaa mpango wa  kuwekeza ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki likilenga kusaidia eneo hilo Kiuchumi.

Alisema mpango huo una nia pia ya kuijumuisha Sudan ambayo  imekuwa ikikabiliwa na  ukame wa mara kwa mara  licha ya kwamba haimo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC }.

“ Tumelenga zaidi kuisaidia Sekta Binafsi kwa vile jamii kubwa  hasa ndani ya Bara la Afrika
 imekuwa ikikabiliwa na Uchumi duni ”. Alisema Bibi Mimi Alemayehou.

Bibi Mimi alifahamisha kwamba  huduma za Shirika hilo la OPIC mara kahaa huelekezwa  katika kutoa  huduma za Kijamii kwenye sekta Binafsi kupitia Makampuni ya Kimarekani Chini ya Shirika la Misaada la Marekani US aid.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi ameuambia Uongozi wa Shirika hilo la Uwekezaji Vitega Uchumi la OPIC kwamba Zanzibar bado inaendelea kutegemea zao moja tu la Uchumi la akARAFUU.

Balozi Seif alisema  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko katika harakati za kuimarisha  miundombinu ili kuyawezesha Makampuni ya  Kigeni kupata fursa ya kuwekeza Zanzibar.
Alisema wawekezaji katika Sekta ya Utalii wana nafasi nzuri ya uwekezaji  kwa vile miundo mbinu ya bara bara, maji na umeme iko katika hatua nzuri.

Hata hivyo Balozi Seif  ameuomba Uongozi wa OPIC kuangalia  uwezekano wa kuanzisha  mradi wa pamoja wa umeme kwa kutumia Nishati ya jua au Bahari ili Zanzibar iwe tayari kukabiliana na  upungufu wa huduma ya umeme hasa wakati kinapopungua kina cha maji  huko Tanzania Bara.

“ Tumekuwa tukipokea  huduma ya umeme  kupitia Gridi ya Taifa  huko Tanzania Bara, lakini wakati mwengine  tunalazimika  kupata umeme wa mgao kutokana na kupungua kwa kina cha maji. Hali hii huathiri utendaji kazi na  kupunguza kasi ya Maendeleo ya Kiuchumi ”. Alisema Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Balozi Seif.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/11/2011.

No comments:

Post a Comment