Thursday, November 3, 2011

SMZ NA TAASISI YA USIRIKIANO YA HOUSTON, MAREKANI KUFANYA UTAFITI KWA PAMOJA UTAKAOPELEKEA KUANZISHWA MRADI WA SAMAKI ZANZIBAR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Taasisi ya Ushirikano ya Jimbo la Houston,Texas Nchini Marekani zimefikia hatua ya kukubaliana kufanya  utafiti wa pamoja utakaopelekea kuanzishwa kwa Mradi mkubwa wa  Samaki  Zanzibar.

Hatua hiyo ya makubaliano imekuja  kufuatia Kikao cha pamoja kati ya Ujumbe wa Zanzibar ulioko Nchini Marekani Kujitanga kwa wawekezaji wa Nchi hiyo ukiongoza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na ule wa Taasisi inayoratibu Miradi mikubwa ya  Samaki Nchini Marekani ya { GRI } ikiongozwa na  Rais wa soko la Kimataifa la Taasisi hiyo Bwana Tomas Newland.

Mazungumzo hayo yamefanyika hapo katika Afisi za Taasisi hiyo kwenye Jimbo la Houston, Texas Nchini Marekani.

Bwana  Tomas Newland  aliueleza ujumbe huo wa Zanzibar kwamba mradi huo mkubwa una uwezo wa kutoa ajira kwa Wananchi zaidi ya thalathini elfu.

Alisema miradi kama hiyo ambayo tayari imeshaanzishwa  katika baadhi ya Mtaifa ya Afrika,Asia, Marekani na Ulaya  inazingatia zaidi uhifadhi wa Mazingira pamoja na utoaji wa mafunzo kwa Wavuvi na Wakulima  wa maeneo ya Vijijini.

“ Miradi kama hii ambayo hufadhiliwa na  Taasisi za Uwekezaji Vitega Uchumi  za OPIC na IFC hugharimu zaidi ya Dola za Kimarekani  Milioni 20,000,000.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  ameshauri kuharakishwa kwa mawasiliano ya pamoja kati ya wataalamu wa pande hizo mbili  ili kuona  wazo hilo la muelekeo wa kuanzishwa  kwa mradi mkubwa wa Samaki linafanikiwa.

Balozi Seif alisema kuanzishwa kwa mradi huo  mbali ya kuleta uhusiano wa karibu kati ya Zanzibar na Marekani  lakini pia utaleta  faraja kwa Wananchi walio wengi kujipatia  ajira ya uhakika.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alikuwa na mazungumzo na Seneta wa Jimbo la Houston,Texas Bwana Rodey Ellis.

Katika mazungumzo yao Senata Rodney aliiponhgeza Zanzibar kwa juhudi zake za  kharaisha Maendeleo ya Kiuchumi.

Seneta Rodney Ellis  amemkabidhi Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake hati Maalum inayompa heshima ya kuwa mkaazi wa Jimbo la Houston, Texas.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/11/2011.

No comments:

Post a Comment