YAH: KAMATI KUU YA CCM KUMWAGIZA RAIS KIKWETE AKUTANE NA VYAMA VINGINE VYA SIASA
Kurugenzi ya Habari na Uenezi imeshangazwa na tamko lililotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ndugu Nape Nnauye kuwa “Kamati Kuu ya CCM imemwagiza Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete akutane na vyama vyote vya siasa badala ya CHADEMA peke yake” aliendelea Kusema kuwa …… “Pamoja na kukubali akutane na CHADEMA, tumetahadharisha kuwa lazima kushirikisha wajumbe wengine kutoka kwenye vyama vyenye uwakilishi ndani ya Bunge isiwe CHADEMA pekee”.
Awali ya yote tunapenda kusisitiza kuwa maridhiano ya kitaifa juu ya mchakato wa kuweza kufikia kupata katiba mpya ni suala ambalo ni la muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu na haswa kama muafaka huo utafikiwa kwa nia njema ya kujenga na kuimarisha mshikamano miongoni mwa watanzania bila kujali dini, rangi, kabila ama itikadi za vyama vyao.
Tamko la Kamati Kuu ya CCM linaonyesha muendelezo wa matamko ambayo wamekuwa wakiyatoa kila mara wanapokutana, mathalani kikao kilichopita kiliiagiza serikali kuwa bei ya mafuta ya taa lazima ishuke, kitu ambacho mpaka leo hakijafanyiwa kazi na hii inaonyesha jinsi ambavyo Kamati kuu hiyo isivyokuwa na msimamo juu ya maamuzi yake na maagizo yake inayotoa kwa viongozi wa kiserikali.
Tamko hili, limetushangaza kwani limeonyesha wazi kuwa kuna hofu miongoni mwa viongozi na wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM kuwa sheria iliyopitishwa na wabunge wa CCM kwa kushirikiana na wale wa CUF haina muafaka wa kitaifa na hivyo wanamwagiza Rais kukutana na makundi mengine ili kupata maoni kabla ya kuisaini sheria hiyo.
CHADEMA tuliandika barua kwa Rais naye alikubali kukutana nasi, kitendo cha Kamati Kuu ya CCM kutoa tamko hili ni dhahiri kuwa kamati kuu ya CCM imejitwalia madaraka ya kuwa wasemaji wa vyama vingine vyenye uwakilishi Bungeni ambao mpaka leo hatujawasikia wakitoa tamko juu ya suala hilo. Tunajiuliza hivi Kamati Kuu ya CCM leo imekuwa ndio wasemaji wa vyama vyenye uwakilishi Bungeni ukiiondoa CHADEMA?
Pili, Vyama vyenye uwakilishi Bungeni ukiiondoa CHADEMA NA NCCR-Mageuzi waliopinga muswada huu, vyama vingine mathalani CUF, CCM na TLP wao waliunga mkono kupitishwa kwa muswada huu, sasa Kamati Kuu ya CCM inataka wakakutane na Rais ili kujadili kitu gani? Wakati walikuwa ni sehemu ya maamuzi ambayo CHADEMA na wadau mbalimbali wanayalalamikia na ndio maana tukataka kuwasilisha malalamiko yetu kwa Rais.
Tunapenda kuikumbusha Kamati Kuu ya CCM kuwa CHADEMA iliomba kukutana na Rais wa Nchi na sio kama Mwenyekiti wa chama, iwapo Rais atakubaliana na agizo hili la Kamati Kuu ya CCM itakuwa dhahiri kuwa ni muendelezo wa ushahidi kuwa viongozi wa Kiserikali wamekuwa wakitimiza majukumu yao kutokana na shinikizo la Chama hata kwenye masuala ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa taifa letu kama suala hili la Katiba lilivyo.
Mwisho, Tungependa kumshauri Rais kuwa pamoja na kukutana na CHADEMA atenge muda ili aweze kukutana na makundi mengine mbalimbali ya kijamii yenye maoni na malalamiko kabla ya kusaini sheria iliyopitishwa na Bunge kwa maslahi ya taifa letu na ili kuweza kuleta utengamano wa kitaifa .Imetolewa na:
Erasto TumboMkurugenzi wa Habari na Uenezi24 Novemba 2011.
No comments:
Post a Comment