Tuesday, November 22, 2011

WAZANZIBARI KWA NAFASI ZAO WATAKIWA KUTUMIA FULSA MUHIMU ILIYOPO KUJADILI MSWADA WA SHERIA

Faki Mjaka na Zahira Bilal-Maelezo, Zanzibar

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Abubar Khamis Bakar amewasihi Wazanzibari kwa nafasi zao watumie fursa muhimu iliyopo kwa sasa kujadili Mswada wa Sheria ya Katiba kwa lengo la kupata Katiba Mpya yenye maslahi ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla. 

Waziri huyo ameyasema hayo leo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Zanzibar alipokuwa akizungumza na Wananchi,Wanasiasa pamoja na Waandishi wa Habari kuhusiana na Mswaada wa Utaratibu wa kupatikana kwa Katiba Mpya.

Amesema upatikanaji wa Katiba Mpya yenye maslahi kwa Wazanzibari inatokana na kuwepo kwa umoja na uzalendo ambao unatanguliza maslahi ya Zanzibar mbele na siyo kujali maslahi ya Vyama.

Abuubakar amewataka pia wananchi wa Zanzibar kujikusanya na kuipitia Katiba iliyopo na kuyajadili mapungufu yaliyomo katika katiba hiyo ili muda utakapofika wa kutoa maoni juu ya Katiba Mpya waweze kufanya hivyo.

Aidha amesema mswaada huo Mpya ambao umepitishwa karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao pia unasubiri kutiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mzuri na wenye kujali maslahi ya Zanzibar.

Waziri huyo wa Katiba na Sheria Zanzibar amewatahadharisha wananchi kuwa makini na watu ambao wanaweza kuwapotosha wananchi katika kipindi hiki cha kujadili mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Amesema kwamba wananchi wanapaswa kuitumia fursa adhimu waliyoipata kipindi hiki na kwamba kama hawatoitumia vizuri wanaweza kuijutia katika maisha yao.

Kwa upande wa wananchi waliochangia katika mkutano huo wamewaomba viongozi na wanasiasa kupita katika Majimbo yao ili kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya upatikanaji wa Katiba Mpya

Aidha wameviomba vyombo vya Habari Zanzibar kuandaa vipindi mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika Makongamano na Warsha mbali mbali juu ya Upatikanaji wa Katiba hiyo

Mkutano huo ambao ulikuwa wa aina yake na kuhudhuriwa pia na baadhi ya Mawaziri wa Seririkali ya Mapinduzi ya Zanzibar wananchi walipata fursa ya kutoa maoni yao juu ya Mswaada huo.

No comments:

Post a Comment