Tuesday, November 8, 2011

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR BADO INAENDELEA NA JUHUDI ZA KUTAFUTA WAWEKEZAJI WA USAFIRI WA BAHARINI

Maalim Seif akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Dini ya Kiislamu waliofika ofisini kwake Migombani. Kutoka Kulia ni sheikh Azani Khalid Hamdani na katibu wa Jumuiya hiyo Sheikh Abdalla Said Ali. (Picha. Salmin Said-OMKR).

Na: Hassan Hamad (OMKR)

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inaendelea na juhudi zake za kutafuta wawekezaji wa usafiri wa baharini ili kukabiliana na tatizo la usafiri lililopo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Hayo yameelezwa na Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo  na ujumbe wa viongozi wa dini kutoka Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu.
Amesema licha ya serikali kuwa na uwezo mdogo wa kununua meli za abiria, lakini inafanya mazungumzo na wawekezaji ili walete meli zenye ubora, na kwamba tayari baadhi ya makampuni yameshaonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo ya usafiri wa baharini.
“Tayari baadhi ya makampuni yameshajitokeza lakini inabidi tufanye uchunguzi ili kubaini ikiwa meli hizo zina ubora unaokubalika na hazijatumika kwa muda mrefu”, amesema Maalim Seif.
Amesema serikali pia inafuatilia tatizo la kuibuka kwa ‘bandari bubu’ ambazo husafirisha abiria na mizigo bila ya kufuata taratibu ili kuepusha uwezekano wa kutokea kwa ajali .
“Serikali iko ‘very strict’ katika suala hili, hatuwezi kukubali kuwaachia watu wakifanya shughuli hizi bila ya utaratibu unaokubalika, ni juzi tu meli ya Seagull ilikuwa imeshazidisha abiria 120 lakini alipigiwa simu Waziri na hatimaye ikabidi washushwe kwenye meli”, alibainisha Maalim Seif.
Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamezungumzia tatizo la usafiri wa baharini hasa katika visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Tanga, tatizo lililojitokeza tangu kusita kwa huduma za Meli za Serikali za Mv. Mapinduzi na Maendeleo, na baadaye Mv. Serengeti na kuzama kwa Meli ya Spice Islanders.
Ujumbe wa viongozi hao ukingozwa na Sheikh Msellem Ali Msellem umesema kwa sasa wananchi wa Zanzibar wanapata usumbufu wa usafiri kutokana na boti zinazotumika kuwa na bei kubwa ambayo wananchi wengi hawaimudu.
Wamesema hali hiyo inapelekea baadhi ya wananchi hasa wafanyabiashara wadogo kusafiri kwa majahazi kuelekea Pemba na Tanga, hali inaweza kuhatarisha usalama wao, hivyo wameiomba serikali kuwa makini katika shughuli za usafiri ili kuepusha uwezekano wa kutokea kwa ajali za baharini.
Kwa upande wake katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Sheikh Abdallah Said Ali ameiomba serikali kuharakisha kuwalipia ada za masomo wanafunzi inaowadhamini katika vyuo mbali mbali ili kuwaondoshea usumbufu wanaoupata.
“Baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakizuiliwa matokeo yao na wengine kuzuiwa kufanya mitihani kwa sababu hawajalipa ada, hii inawaathiri sana wanafunzi” alidai Sheikh Abdallah.
Viongozi hao wa dini pia wameishauri serikali kupitia Wizara ya afya kuzingatia mazingira ya wagonjwa wanaofika hospitali, ili kuwapatia huduma badala ya kuweka maslahi mbele.
Wamedai kuwa baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kucheleweshwa kupatiwa huduma kwa sababu hawana malipo stahiki, na kushauri wapatiwe huduma kwanza ndipo yafuate malipo ili kuokoa maisha ya wananchi.

No comments:

Post a Comment