Na Nafisa Madai Maelezo -Zanzibar
WAZIRI wa Sheria na Katiba, Abubakari Khamis Bakary, amesema kasi ya wataalamu wanaokimbilia sekta binafsi, imekuwa na athari kubwa katika kuleta ufanisi na mageuzi katika sekta ya umma.
Hayo aliyaeleza wakati akifungua warsha ya maendeleo ya rasilimali watu kwa wataalamu wa Shirikisho la Mawasiliano la Kusini mwa Afrika (SATA), kwaniaba ya Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano na Uchukuzi huko katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View mjini zanzibar.
Waziri huyo alisema baadhi ya watu wanaona utaratibu huo ni njia muafaka kwa kuwa watalaamu wanapata fursa ya kuchangia ujuzi wao katika sekta zote za uchumi.
Waziri Bakary, alisema mtazamo huo unahitaji kuungwa mkono na wote kwa kuwa sekta binafsi na umma zina nafasi sawa katika ujenzi wa uchumi katika mataifa hayo.
Alisema Zanzibar kama sehemu ya dunia imekuwa ikipoteza wataalamu wake wengi, wanaokwenda kufanya kazi katika nchi nyengine, wakitafuta uzoefu na maslahi zaidi.
Waziri Bakary alisema hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuwadhibiti au kuwafungia wataalamu wake wasitoke ndani ya nchi zao, lakini kama nchi wanachohitaji kukifanya ni kutengeneza fursa za ajira pamoja na kulipa mishahara mizuri kwa ajili ya wataalamu wa ndani.
Naye Mtendaji Mkuu wa Posta Tanzania, Said Amir.Said alisema, teknolojia ya mawasiliano imekuwa ikibadilika haraka sana hivyo lazima wataalamu wa mawasiliano nao kubadilika kwa ajili ya rasilimali watu.
Aidha alieleza mkutano huo umekuwa fursa nzuri kwa Zanzibar kutambulika wakati huu mkonga wa mawasiliano ukitarajia kuchukua nafasi katika visiwani vya zanzibar
Jumla ya wataalamu wa nchi 10 za Shirikisho la SATA walishiriki katika mkutano huo zikiwemo Msumbiji, Botswana, Namibia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Malawi, Zambia na Tanzania.
Mkutano huo wa siku tatu ambao unatarajiwa kufungwa leo hii wataalamu hao wataweza kupata fursa ya kutembelea maeneo kadhaa ya mji wa zanzibar ikiwemo kizimbani ambako watakagua mashamba ya spice, mji mkongwe.
No comments:
Post a Comment