Kamishna wa polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa akitoa rai mbele ya makamu wa kwanza wa Rais maalim Seif Sharif hamad katika kufanikisha operesheni za kutokomeza mifuko ya Plastiki Zanzibar.
Maalim Seif akizungumza na kikosi kazi cha kupambana na mifuko ya plastiki ukumbi wa mikutano katika OMKR Migombani.(Picha, Salmin Said- OMKR)
Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar maalim Seif Sharif Hamad amesema mashirikiano zaidi yanahitajika katika kutokomeza matumizi ya mifuko ya plastiki Visiwa Zanzibar.
Sambamba na hilo Maalim Seif amesisitiza elimu zaidi itolewe kwa wananchi ili kutambua athari za matumizi ya mifuko hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa chanzo kikuu cha uchafu katika manispaa ya mji wa Zanzibar.
Maalim Seif alikuwa akizungumza na kikosi kazi cha kupambana na matumizi ya mifuko ya plastiki huo Ofisni kwake migombani, kinachowashirikisha watendaji 10 wakiwemo kutoka jeshi la polisi, Wizara ya Biashara na idara ya Mazingira.
Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana tangu kikosi kicho kizinduliwe rasmi na kuanza kazi miezi michache iliyopita, bado juhudi zaidi zinafaa zichukuliwe kwa kulishirikisha kikamilifu jeshi la polisi katika operesheni zinazofanywa za kuisaka mifuko ya plastiki na kuifanya Idara ya mazingira kuwa mratibu mwezeshaji wa operesheni hizo.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Mhe. Fatma Abdulhabib Fereji ambaye alishiriki katika mazungumzo hayo amesema ni vyema kikosi hicho kikaangaliwa upya ili kutoa fursa kwa jeshi la polisi kuongoza operesheni hizo.
Mhe. Fereji pia ameahidi kusimamia kanuni za sheria ya kutoa adhabu kwa watu watakaopatikana na mifuko hiyo ambayo kwa ujumla inakaribia kukamilika na kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali ili iweze kufanya kazi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na kamishna wa polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa amesema bado kuna fursa nzuri ya kufanikiwa kwa operesheni hizo iwapo zitawahusisha viongozi wa shehia na kutekeleza mpango wa polisi jamii katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Watendaji wa kikosi hicho kwa upande wao wameelezea changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi hasa usafiri, pamoja na kutokuwepo sheria madhubuti ya kuwahukumu wanaokamatwa na mifuko hiyo.
Wamesema hali hiyo inawafanya wananchi kutokuwa na hofu kwa vile hakuna sheria inayowabana, na hivyo kulifanya zoezi hilo kuwa gumu.
Kikosi kazi hicho kimeiomba serikali kusimamia utekelezaji wa maagizo yake katika mamlaka zinazohusika, wakidai kuwa mifuko mingi kati ya inayoingia nchini inapitia katika bandari kuu ya Zanzibar huku watendaji wa mamlaka hiyo wakifumbia macho agizo hilo.
No comments:
Post a Comment