Thursday, November 24, 2011

SMZ YAKUSUDIA KUKIENDELEZA CHUO KIKUU SUZA KIWE MFANO AFRIKA MASHARIKI NA AFRIKA NZIMA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Taifa cha Zanzibar SUZA Profesa Idrisa Rai akimueleza Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad malengo ya chuo hicho huko OMKR migombani.

Hassan Hamad (OMKR).

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imesema inakusudia kukiendeleza Chuo Kikuu Cha Taifa SUZA ili kiwe mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki na Bara zima la Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake migombani alipokutana na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Idrisa Rai.

Amesema inawezekana kwa chuo hicho kupata mafanikio makubwa kutokana na mipango yake imara ya kuimarisha miundombinu ya majengo pamoja na kuanzisha vitivo mbali mbali vya masomo yanayokwenda na wakati.

Ameuomba uongozi wa chuo hicho kufikiria pia kuanzisha kituo cha utafiti wa kilimo hasa kwa zao la karafuu ikizingatiwa kuwa hilo ni zao tegemeo katika uchumi wa Zanzibar.

Aidha ameunga mkono malengo ya chuo hicho kuweka msisitizo katika taaluma ya habari na mawasiliano ICT kwani ina mchango mkubwa katika maendeleo ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Idrisa Rai amesema Chuo hicho kinakusudia kupanua huduma zake kwa kuingiza taaluma mbali mbali ambazo zitasaidia maendeleo ya jamii.

Amezitaja baadhi ya taaluma hizo kuwa ni pamoja na utalii, kilimo, habari na mawasiliano, sambamba na kutoa mafunzo ya ngazi ya shahada ya pili na tatu kwa fani ya Kiswahili.

Amesema Chuo kimezingatia umuhimu wa kuliendeleza somo la Kiswahili ikizingatiwa kuwa Zanzibar ndio kitovu cha lugha hiyo ambayo mahitaji yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi dunia.

Amesema wanakusudia kuitangaza lugha hiyo ili kila mgeni atakayehitaji kujifunzi lugha hiyo afike Zanzibar badala ya kwenda nchi nyengine na kwamba mafanikio ya Kiswahili yataitangaza Zanzibar kiutalii duniani kote.

Aidha Profesa Rai amesema chuo hicho pia kina malengo ya kuwaendeleza wakufunzi wake kwa kuwapa elimu ya kiwango cha juu ili waweze kuisambaza elimu hiyo kwa wanafunzi, na kukifanya chuo hicho kiwe na sifa ya kujivunia ya kutoa elimu bora ambayo pia itanyanyua kiwango cha elimu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment