Monday, November 21, 2011

SMZ KUSHIRIKIANA NA WANAWAKE WATAALAMU WA KILIMO NA MAZINGIRA NCHINI KUINUA HALI ZA MAISHA YA WANAWAKE

Maalim Seif akifungua mkutanao wa 15 wa mwaka wa Jumuiya ya TAWLAE.
Maalim Seif akisalimiana na viongozi na wanachama wa TAWLAE katika hafla ya ufunguzi ya mkutano wa 15 wa Jumuiya hiyo ya wanawake. 

Na Hassan Hamad, OMKR                              
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali itashirikiana kikamilifu na wanawake wataalamu wa Kilimo na Mazingira nchini katika kuhakikisha jamii inaelewa umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kuinua hali za maisha ya wanawake.
Maalim Seif amesema hayo leo alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Wanawake Wataalamu wa Kilimo na Mazingira (TAWLAE) huko katika ukimbi wa mikutano wa EACROTANAL mjini Zanzibar.
Maalim Seif amesema kazi zinazofanywa na jumuiya hiyo za kuwaelimisha wanawake kuhimiza matumizi ya nishati mbadala na uhifadhi wa mazingira, kuwatoa watoto kwenye ajira mbaya na kuwasomesha zinaungwa mkono na serikali na kuna haja jumuiya na mashirika mengine yaziunge mkono.
Alisema majukumu hayo ni muhimu katika kuwaletea maendeleo wanawake na kuinua maisha ya wananchi kwa ujumla kwasababu kumsaidia mwanamke ni sawa na kuisadia jamii nzima.
Alisema suala la kuhimiza matumizi ya nishati mbadala ni jambo la kupewa umuhimu wa kipekee hasa kwa vile dunia hivi sasa inashuhudia athari kubwa zilizosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameathiri maisha ya watu wengi pamoja na kudidimiza uchumi wa nchi.
“Endeleeni na juhudi hizi za kueneza elimu na kuinua uelewa wa wanawake na jamii yetu, serikali zinakuungeni mkono, kwasababu tunajua mikakati hii itapelekea kuokoa mazingira yetu yasiathiriwe lakini pia zitachangia kwa kiasi kikubwa maisha ya wanawake na jamii yote kuwa bora zaidi”, alisema Maalim Seif.
Sambamba na hatua hizo zinazochukuliwa, Makamu wa Kwanza wa Rais ameishauri TAWLAE kushirikiana bega kwa bega na wadau wengine katika kupiga vita matumizi, uingizaji na usambazaji dawa za kulevya, ili kutoa mchango wao katika kuyaokoa maisha ya vijana waliojiingiza katika janga hilo, wakiwemo wasichana.
“Nashauri TAWLAE pia ijikite katika kuwaokoa vijana, hasa vijana wa kike waliozama katika matumizi ya madawa ya kulevya kwa kuwa na mipango thabiti ya kuwapatia matibabu vijana hao na kasha kuwasaidia kupata ajira”, alishauri Maalim Seif. 
Alisema kwa upande wa Zanzibar katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na kuwasaidia wale waliojiingiza kwenye matumizi yake, juhudi kubwa zinaendelea kuchukuliwa, ikiwemo kujengwa nyumba za kuwapa ushauri na kuwarekebisha kitabia vijana hao (Sobber Houses), ambapo vijana wa kike na kiume wananufaika na ushauri pamoja na huduma mbali mbali.
Mapema Mwenyekiti wa TAWLAE, Christine Lyimo alisema pamoja na mafanikio ya kuwasomesha wanawake katika ngazi mbali mbali, bado TAWLAE kinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uwezo mdogo wa kuendeleza wanawake wengi zaidi na tatizo la baadhi ya wanachama kuchelewa kulipa ada zao.
Wakati huo huo Makamu wa kwanza wa Rais amelitaka Baraza la Manispaa Zanzibar kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na jeshi la polisi katika kudhibiti mifugo inayozurura katika manispaa ya mji wa Zanzibar.
Amesema mifugo hiyo imekuwa ikileta kero katika mji ikiwa ni pamoja na kuchafua mazingira ya mji na kusababisha ajali, ambao ambayo yanaweza kuepukwa iwapo mifugo hiyo itadhibitiowa.
Akichangia katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Migombani, kamishna wa polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa amependekeza kuzingatiwa ushirikishwaji wa wananchi kupitia polisi jamii katika kukabiliana na tatizo hilo.
Pia kamishna Mussa amependekeza kukabiliana na chanzo cha kuzagaa kwa mifugo hiyo ambacho ni mazizi ya mifugo katika eneo la mjini, na kwamba kufanya hivyo kutarahisisha kuondoa tatizo la kuzagaa kwa mifugo katika eneo la mjini.

No comments:

Post a Comment