Tuesday, November 22, 2011

WANANCHI WA ZANZIBAR WAMEPATA MWAMKO MZURI KATIKA VITA DHIDI YA MAAMBUKIZI MAPYA YA VIRUSI VYA UKIMWI: SMZ

Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais anayehusika na mambo ya UKIMWI Mhe. Fatma Abdulhabib Fereji akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar ZAC Dr. Omar Makame Shauri katika mazungumzo na Waandishi wa ahabri juu ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yanayofikia kilele chake Disemba 01, 2011.
Mhe. Fatma Ferej akizungumza na waandhishi wa habari juu ya maadhimisho.
Mhe. Fatma Ferej akizungumza na waandhishi wa habari juu ya maadhimisho.
Waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali nchini wakisikiliza hotuba ya Mhe. Fatma Ferej kuhusiana na maadhimisho ya ya siku ya Ukimwi duniani. Hafla hiyo ilifanyika OMKR Migombani Zanzibar. (Picha, Salmin Said, OMKR).

Na: Hassan Hamad. (OMKR)

Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar  imesema wananchi wa Zanzibar wamepata  mwamko mzuri katika vita dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na Unyanyapa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo.
Akizindua wiki ya kampeni ya maadhimisho ya siku wa UKIMWI duniani itakayofikia kilele chake tarehe 01 Disemba 2011 duniani kote, Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej amesema mafanikio hayo yametokana ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na Tume ya UKIMWI Zanzibar katika mapambano hayo.
Mhe. Fatma Fereji alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali ofisini kwake kufuatia maadhimisho hayo yatakayoadhimishwa kitaifa katika kijiji cha Makombeni, Wilaya ya Mkoani Pemba ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohd Shein.
Amesema kwa sasa idadi ya maambukizi inabakia kuwa asilimia 0.6 kwa Zanzibar lakini kuna  makundi matatu ya vijana yameathirika zaidi. “Ukweli hali ya maambukizi kwa ujumla ni asilimia 0.6, lakini hali ni mbaya kwa watumiaji wa dawa za kulevya hasa wanaojidunga sindano ambao wameambukizwa kwa asilimia 16, kundi la wanawake wanaojiuza asilimia 10.8 na watu wanaofanya mapenzi ya jinsi moja asilimia 12”, alifafanua Mhe. Fereji.
Amefahamisha kuwa juhudi zaidi zinapaswa kuchuliwa ili kufikia wito wa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ambayo ni “Kuzifikia Sifuri tatu”, ikiwa na tafsiri ya kufikia asilimia zero ya maambukizi mapya, asilimia zero ya unyanyapaa na asilimia zero ya vifo vitokanavyo na UKIMWI ifikapo mwaka 2015.
Amesema kauli mbiu hiyo inaweza kufikiwa iwapo wadau wote wakiwemo wananchi watashirikiana katika kuondoa muhali wa kuwafichua watumiaji wa dawa za kulevya na kuhamasika kupima afya kila baada ya kipindi fulani.
“muhali ndio unaotuharibia wazanzibari, lakini ikiwa tutaondoa muhali kuwafichua watu hawa na kuepukana na unyanyapaa wa aina zote, bali malengo hayo ya sifuri tatu yatafikiwa”, alisema.
Amebainisha kuwa hali ya unyanyapaa imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita, hali inayopelekea baadhi ya wachumba kukubali kufunga ndoa, huku mmoja kati ya wapenzi hao akiwa ameathirika.
Ametoa wito kwa jamii ya kizanzibari kufuata maadili yao ambayo ndio kinga pekee ya maambukizi mapya, akitoa mfano kuwa makundi yote matatu yaliyoathirika zaidi yanafanya mambo hayo kinyume na maadili ya Wazanzibari na dini.
Mhe. Fereji amekwenda mbali zaidi pale akipotoa onyo la kumuwajibisha mtendaji yeyote wa Ofisi yake atakayebainika kuendeleza unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi ya VVU.
Akizungumza katika kikao hicho na waandishi wa habari, Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya UKIMWI Zanzibar ZAC Dr. Omar Makame Shauri amesema kiasi ya shilingi milioni 30 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya maadhimisho hayo.
Amesema licha ya mafanikio yalioyopatikana, lakini bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi kushindwa kubadili tabia na kuendeleza unyanyapaa, jambo ambalo tume yake inajaribu kutoa elimu kwa wananchi ili kutoa uelewa zaidi ya tatizo hilo.
Dr. Shauri ametoa wito kwa wananchi kuvitumia vituo vya ushauri nasaha na kupima VVU bila ya malipo, ili kutambua maendeleo ya afya zao kwa lengo la kuepusha maambulizi ya VVU na vifo vitokanavyo na janga hilo.

No comments:

Post a Comment