Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar maalim Seif Sharif Hamad akipokea zawadi ya kompyuta ya dijital kutoka kwa Naibu Waziri wa mawasiliano ya Habari wa China Li Wei katika shamrashamra za uzinduzi wa kampuni ya Star Times ya China ambayo imepewa leseni kuendesha shughuli zake za matangazo ya Televisheni kwa dijital hapa Zanzibar.
Maalim Seif akizungumza katika uzinduzi wa kampuni ya Star Times ya China huko Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Zanzibar.
Maalim Seif akipongezana na Naibu Waziri wa habari wa China baada ya uzinduzi wa kampuni ya Star Times. Kulia ni Waziri wa habari, utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Abdillahi Jihadi Hassan. (Picha, Salmin Said- OMKR).
Hassan Hamad (OMKR)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa kibali rasmi cha kuiruhusu kampuni ya Star Times ya China kuendesha shughuli zake za matangazo ya televisheni kwa kutumia mfumo wa kisasa wa dijital.
Akizindua mpango huo huko hoteli ya Zanzibar Beach Resort Zanzibar, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwepo kwa kampuni hiyo kutakuza ushirikiano wa muda mrefu kati ya China na Zanzibar.
Ameitaka kampuni hiyo kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia maadili ya wazanzibari sambamba na kufuata sheria za nchi, na kwamba serikali itafanya kazi bega kwa began a kampuni hiyo katika kuhakikisha kuwa inaendesha shughuli zake bila usumbufu.
Amesema licha ya kampuni hiyo kuwepo kibiashara, lakini itasaidia kutoa ujuzi kwa wazalendo, pamoja na kutoa nafasi za ajira kwa vijana wa Zanzibar ambao wengi wao wanasomea sekta ya habari bila ya uhakika wa ajira zao.
Amefahamisha kuwa China ni rafiki wa kweli wa Zanzibar na kwamba serikali inathamini sana mchango wa nchi hiyo katika nyanja mbali mbali za maendeleo na bado inakaribisha makampuni zaidi ya kichina kuja kuwekeza miradi yao.
Ameiomba kampuni hiyo pia kuzingatia hali ya uchumi wa Zanzibar, ili waweke viwango vya malipo ambavyo wazanzibari wengi wataweza kuvimudu na kuitumia televisheni hiyo kwa kupata taaluma na burudani zitakazotolewa.
Kampuni ya Star Times ya China ni kampuni ya mwanzo ya kigeni kuruhusiwa kuendesha shughuli hizo za habari hapa nchini, lakini tayari inaendesha shughuli zake kwa mikoa saba ya Tanzania Bara na ina wateja wapatao 140,000.
Mwenyekiti wa kampuni hiyo Pang Xin Xing amesema leseni hiyo ni hatua muhimu katika kufikia matarajio yao ya kukuza ushirikiano na kuelimisha jamii juu ya mambo mbali mbali ya maendeleo, tamaduni na kukuza biashara.
Kabla ya uzinduzi huo Makamu wa kwanza wa Rais alikutana na Naibu Waziri wa mawasiliano ya habari wa China Bw. Li Wei ambaye ameelezea matumaini yake ya kuendelea kwa uhusiano wa muda mrefu baina ya pande hizo mbili.
Bw. Li amesema ushirikiano uliopo haulengi baina ya serikali kwa serikali pekee bali unatapakaa katika nyanja mbali mbali zikiwemo vyombo vya habari wakati ambapo tayari matangazo ya Televisheni ya taifa ya China ya CCTV News na yale ya Radio China Kimataifa CRI yanapokelewa vizuri na wananchi wa Zanzibar.