Tuesday, November 8, 2011

UINGEREZA INAFURAHISHWA NA ZANZIBAR - PRINCE CHARLES

Na Salama Njani Habari Maelezo Zanzibar 

Imeelezwa kuwa Zanzibar ni sehemu moja wapo yenye mashirikiano mazuri na Uingereza katika Nyanja mbali mbali za kimaendeleo kama mataifa mengine duniani.
 
Hayo yameelezwa na mtoto wa Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza Prince Charles, alipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Ali Mohammed Shein, Ikulu mjini Zanzibar alipokwenda kumsalimia baada ya kuwasili akitokea jijini Dar es Salaam.
 
Amesema kuwa Uingereza inafurahishwa na Zanzibar juu ya juhudi zilizopo za kukuza ushirikiano kati ya nchi mbili hizi, na ameahidi kuwa Uingereza itahakikisha inaimarisha mashirikiano yaliopo kwa lengo la kuleta maendeleo.
 
Prince Charles akiambatana na mkewe Duchess of conrnwall, pamoja na ujumbe wao waliwasili uwanja wa ndege wa zanzibar na kupokelewa na Makamo wa a Pili wa Rais wa Zanzibar,Balozi Seif Ali Iddi pamoja na viongozi wengine wa serikali.
 
Katika ziara yake ya kutwa moja Prince Charles alipata nafasi ya kukutana na Rais mstaafu wa awamu ya sita wa zanzibar DK Amani Abeid Karume na kutembelea sehemu za kihistoria na kuona vivutio mbali mbali vya utalii pamoja na sanaa ya wazanzibari.
 
Miongoni mwa sehemu alizotembelea ni pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar, makumbusho ya Beit el ajaib, mashamba ya viungo vya zanzibar pamoja na kutembelea miradi mbali mbali ambayo inadhaminiwa na serikali ya Uigereza.
 
Aidha katika ziara hiyo alitoa msaada wa vyandarua kwa wizara ya Afya ambavyo vilikabidhiwa kwa katibu mkuu wa wizara hiyo DK Saleh Jidawi.

No comments:

Post a Comment