Monday, November 21, 2011

SEKTA YA UVUVI NA KILIZO ZITAPATA MAFANIKIO MAKUBWA IWAPO MIPANGO ILIYOPO ITATEKELEZWA

Maalim Seif akizungumza na wananchi wa kisiwa cha UZI wilaya ya kati Unguja alipofanya ziara ya siku moja katika kisiwa hicho. Alizungumzia masuala mabli mbali yakiwemo utunzaji wa mazingira, uvuvi haramu na UKIMWI.(Picha, Salmin Said-OMKR) 

WILAYA YA KATI  
Na: Hassan Hamad (OMKR)                                   
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema sekta za uvuvi na kilimo zitapata mafanikio makubwa iwapo mipango iliyopo inatatekelezwa kama inavyotarajiwa.
Amesema kampuni kadhaa zinatarajiwa kuwekeza katika shughuli za mazao ya bahariri ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vya usindikaji wa samaki kwa lengo la kuinua kipato cha wavuvi hasa wadogo wadogo.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kisiwa cha Uzi katika Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja alipofanya ziara ya siku moja katika kisiwa hicho.
Amefahamisha kuwa makampuni mengi yanavutiwa na shughuli za uvuvi na kwamba kuna mpango wa kujengwa kwa viwanda vitakavyotengeneza boti za kisasa za uvuvi hapa Zanzibar ambavyo vitawasaidia wavuvi kujiendeleza na kuwa na uwezo wa kuvua katika bahari kuu.
Amesifu mchango wa wananchi wa kisiwa hicho katika kukabiliana na uvuvi haramu na kutaka waendeleze jitihada hizo ili kulinda mazalio ya samaki na kujenga mazingira bora ya kuongeza kipato chao kupitia mazao ya baharini.
“Nakupongezeni sana wananchi wa Uzi kwa jinsi mnavyojitahidi kukabiliana na uvuvi haramu, najua mnakabiliwa na vikwazo katika kufanya hivyo, lakini tutajitahidi kuwa pamoja nanyi ili kuviepuka vikwazo hivyo”, alisema Maalim Seif.
Kwa upande mwengine amewapongeza wananchi wa kisiwa hicho kwa utunzaji wa mazingira na kuwataka waendeleze ulinzi ili kuwapigavita waharibifu wa mazingira hasa ukataji wa mikoko, na kuwasisitiza kupanda miti pale wanapoona mikoko imepungua kwa lengo la kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais pia alitumia fursa hiyo kuwaasa wanakisiwa hao kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kwani janga hilo halina tiba na kutoa wito kufutwa kwa maadili ya kiislamu katika kukabiliana na janga hilo.
“Maadili ya dini ya kiislamu yanaelekeza vijana waliofikia umri na wenye uwezo waowe, lakini bado vijana wengi hawajaitikia wito huu”, alisisitiza Maalim Seif na kuwaomba vijana waowe ili kujikinga na janga hilo.
Katika risala yao iliyosomwa na diwani mstaafu wa wadi ya Uzi Ali Hussein Mrisho wananchi wa kisiwa hicho wameiomba serikali kuwasaidia ili waweze kunufaika na matunda ya visiwa vya Pungume na Nyemembe ambavyo vilikuwa chini ya kisiwa mama cha Uzi.
“Mhe, Makamu wa kwanza wa Rais, tunaiomba serikali itusaidie kwa hili kwani kwa sasa hatufaidiki na chochote kutoka kwenye visiwa hivi ambavyo zamani vilikuwa ni mali yetu” alisema Mrisho.
Akijibu hoja hiyo Makamu wa kwanza wa Rais aliwaahidi wananchi wa kisiwa cha Uzi kulifanyia kuyafanyia kazi malalamiko hayo ili kujiulikana mstahili wa visiwa hivyo vidogo vidogo.

No comments:

Post a Comment