Tuesday, November 22, 2011

TANZANIA NA CHINA ZATIA SAINI MIKATABA MITATU YA MIRADI YA MAENDELEO

Na Bebi Kapenya
MAELEZO, Dar es Salaam

SERIKALI ya Tanzania na ile ya China wamewekeana saini ya mikataba mitatu ya miradi mbalimbali ya maendeleo isiyo na riba yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 89.7 pamoja na kubadilishana hati ya ujenzi wa kituo cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere.

Hafla hiyo imefanyika jana Jijini Dar es Salaam, ambapo Serikali ya Tanzania imewakilishwa na Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo na kwa upande wa China imewakilishwa na Naibu Waziri wa Biashara wa nchi hiyo Jiang Yaoping.
 
Mikataba hiyo iliyosainiwa ni katika sekta za mawasiliano pamoja na ile ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii pia makabadhiano ya hati ujenzi wa kituo cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere kinachotarajiwa kukamilika mwezi Mei mwakani.

Waziri Mkulo aliishukuru Serikali ya watu wa China kwa mkopo huo na kuwahakikishia kwamba Tanzania itatumia fursa hiyo kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo yaliyokusudiwa.
Waziri aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania imeshatenga ardhi kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa kituo cha Mwalimu Nyerere na kuongeza kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni fedha kwa ajili ya fidia kwa wakazi wa eneo husika.
 
Aidha Waziri Mkulo alisema, Serikali itashirikiana na Ubalozi wa China nchini ili kuhakikisha usalama wa watu wa China unakuwepo na kwamba watawashughulikia wale wote walio husika katika mauaji ya mfanyabiashara wa kichina yaliyotokea hivi karibuni.

Kuhusu madeni ya wakandarasi wa Kichina wanaofanyakazi hapa nchini Waziri Mkulo amemuahidi kiongozi huyo kulishughulikia haraka iwezekanavyo, hivyo amewataka kuendelea kuwa wavumilivu huku wakiendelea na shughuli zao.

Kwa upande wake Jiang Yaoping alisema, Serikali ya China itaendelea kuisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kuiomba serikali itumie misaada hiyo inavyotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment