Monday, November 21, 2011

KUTOKA BLOGU YA JAMII: PROFESA CHRIS MAINA PETER ACHAGULIWA KUWA MJUMBE WA KAMISHENI YA SHERIA ZA KIMATAIFA ZA UMOJA WA MATAIFA

maafisa, kutoka kushoto, Bw. S. Shilla na Bw. Assah Mwambene kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Kimataifa,  wakiwa na  Kaimu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dr. Justin Seruhere  wakipongezana baada ya  Profesa Chris  Maina Peter  kutangazwa kuwa ni mmoja kati ya wagombea tisa kutoka kundi la  Afrika walioshinda  uchanguzi wa kuwania nafasi ya  ujumbe wa Kamisheni ya  Umoja wa mataifa  inayoshughulikia  sheria za kimataifa. katikati ni Bi  Tully Mwaipopo akijaribu kumtafuta kwa simu Profesa Maina  ili kumpatia habari njema za ushindi wake katika uchaguzi huo ambao kura zake zilipigwa kwa siri. Jumla ya wagombea 34 kati ya 49   wakiwakilisha mabara mbalimbali walishinda katika uchaguzi huo.
Afisa   mshauri wa masuala ya sheria na uchaguzi katika Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa,  Bi, Tully Mwaipopo akiendelea na  kampeni ya  kugawa vipeperushi vyenye wasifu wa  Profesa Chris Maina Peter aliyekuwa akigombea nafasi ya  ujumbe katika  Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya sheria za Kimataifa, katika uchaguzi uliofanyika  siku ya Alhamis katika ukumbi Mkuu wa  Mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. New York

Na Mwandishi Maalum,New York


Profesa Chris Maina Peter, Muhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amechaguliwa kuwa mjumbe wa  Kamisheni ya  Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Sheria  za Kimataifa ( International  Law Commission).

Wajumbe wa  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  katika mkutano wao  uliofanyika siku ya Alhamis,  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini  New York. Walipiga kura ya siri  kuwachagua  wajumbe 34 kati ya  49 waliotakiwa  kuingia katika Kamisheni hiyo.

Rais wa Baraza Kuu la  66 la  Umoja wa Mataifa, Balozi Nassir Abdulaziz Al- Nasser alimtaganza   Profesa Chris Maina Peter    kutoka Tanzania,  kuwa ni mmoja ya    wagombea Tisa kati ya Kumi na Tatu  kutoka  Afrika  ambao wameshinda na hivyo  kuingia  katika Kamisheni hiyo.

Profesa Chris Maina Peter  ameshinda uchaguzi huo, uliokuwa na ushindani mkubwa akichuana na wagombea wengine 13 waliosheheni sifa na weledi wa hali ya juu katika nyaja ya sheria za kimataifa wakiwamo mabalozi na watu mashuhuri kama  aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya Bw. Amos S. Wako.

Wagombea wengine mbali ya wale tisa kutoka Afrika, walikuwa ni    Nane kutoka  kundi la nchi za Asia,  Watatu kutoka kundi la  Ulaya Mashariki, Sita kutoka kundi la  Amerika ya Latini na Visiwa vya  Caribbean na Wanane kutoka nchi za  Ulaya ya Magharibi  na nchi nyingine.

Profesa  Chris Maina Peter, atakuwa mjumbe wa Kamisheni hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Januari 2012.

Katika kiny’anga’nyiro hicho,  wagombea kutoka kundi  A ambalo ni Afrika lilikuwa na wagombea  13 lakini waliotakiwa ni 9 tu hali iliyopelekea ushindani mkubwa na hasa ikizingatiwa kwamba, kati ya wagombea hao 13 , sita walikuwa wakiomba kurejea tena kwa mara ya pili.

Mbali  ya Tanzania, wengine kutoka Kundi la Afrika walioshinda ni  wagombea kutoka Afrika ya Kusini, Egypt,  Msumbiji, Nigeria, Algeria, Kenya,Libya na Cameroon.

Ushindi wa Profesa Chris Maina Peter umetokana  kwanza, uthubutu, wasifu,na weledi binafsi wa Profesa Maina, uratibu na ushirikiano mkubwa  kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa ambako,  maafisa wake wakiongozwa na  Balozi wao Mhe. Ombeni Sefue, walifanya kazi kubwa na maandalizi mazuri ya kufanikisha uchaguzi huo.

Profesa  Chris Maina Peter yeye binafsi, akiongozwa na Afisa wa Ubalozi wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa,anayehusika na  Kamati ya  Sita ya Masuala ya Sheria na Uchanguzi alifanya kampeni kwa takribani wiki zima akikutana na Mabalozi na Maafisa mbalimbali  hapa Umoja wa Mataifa.

Akizungumza wa njia ya simu kutoka  Addis Ababa Ethiopia, Profesa  Chris Maina Peter amesema, ameyapokea matokea hayo kwa furaha kubwa  huku akiwashukuru wale wote waliofanikisha  uchaguzi huo.

Ushindi wa Profesa Peter unakuja ikiwa ni takribani wiki moja tangu Balaza Kuu la Umoja wa Mataifa  kumthibitisha Mdhibiti na  Mkaguzi wa Hesabu za Serikali,  (CAG) Bw. Ludovic Utouh   kuwa mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa (UNBOA).

Tanzania kupitia Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania  NAOT imeteuliwa kujaza nafasi  itakayoachwa  wazi mwakani na Afrika ya Kusini katika UNBOA. Bw. Ludovic Utouh atafanya kazi na wajumbe wengine wa bodi hiyo kutoka China na Uingereza.

No comments:

Post a Comment