Sunday, October 9, 2011

VIONGOZI WA MAJIMBO KUPITIA CHAMA CHA WANANCHI CUF WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA PAMOJA

Maalim Seif akizungumza na wajasiriamali wanawake wa eneo la Bweleo alipotembelea  vikundi hivyo jana.
Mmoja wa wamiliki wa mradi wa ufugaji kamba Bweleo MAJID SOUD alimuonesha Maalim Seif kama wanaowafuga na kuwasafirisha nje ya nchi (Picha na Salmin Said (OMKR)

Na: HASSAN HAMAD (OMKR)
Viongozi wa majimbo kupitia chama cha wananchi cuf wamehimizwa kufanya kazi kwa pamoja sambamba na kuwa karibu na wananchi ili kuwaletea maendeleo ya haraka wapiga kura wao.
 
wito huo umetolewa na katibu mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa akifungua semina kwa wabunge na wawakilishi wa chama hicho iliyofanyika ukumbi wa baraza la wawakilishi mbweni.
 
Amesema mashirikiano mazuri kati ya wabunge, wawakilishi na madawani yatarahisisha kazi ya kuwatumikia wananchi ambao ni wadau muhimu katika harakati za kuikomboa nchi kiuchumi.
“Viongozi mnaposhikamana mkawa kitu kimoja na wananchi watashikamana, na mkianza kugawana kila mmoja atapata wafuasi na chama kitagawanyika”, aliwaambia viongozi hao.
 
Amesema mwaka mmoja tayari umepita tangu uchaguzi mkuu wa mwaka jana ufanyike na kuwataka viongozi hao kujitahmini ili kuukabili uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wakiwa kitu kimoja.
Aidha Maalim Seif amesifu mafanikio yaliyopatikana katika vikao vilivyopita  na kuwataka viongozi hao kufanya utafiti wa kina kabla ya kuingia kwenye vikao ili kutoa hoja zitakazokiimarisha chama hicho na kuwasaidia wananchi.
 “Wakati umefika kwa Wawakilishi na Wabunge kutumia mtandao kutafuta taarifa na asiyejua aanza sasa”, aliwasisitiza viongozi hao
Kwa upande mwengine Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka viongozi hao kuweka bajeti ya muda ili waweze kupanga muda wao na kuwatembelea wananchi, sambamba na kushiriki katika shughuli za kijamii zikiwemo maziko na harusi.
 
Wabunge na Wawakilishi hao wamejadili mada mbili ambazo ni (Wajibu wa Mwakilishi na Mbunge kwa Chama na wananchi na Kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015)
Wakati huo huo Makamu wa kwanza wa Rais ametembelea maeneo mbalimbali kuangalia shughuli zinazosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zikiwemo mradi wa ufugaji wa kamba na vikundi vya wajasiriamali mali wanawake wanaotumia rasilimali za baharini.
 
Mmoja wa wamiliki wa kituo cha ufugaji kamba cha Bweleo ambao zaidi husafirishwa nje ya nchi Bw.  MAJID SOUD amesema soko la bidhaa hiyo ni kubwa ndani na nje ya nchi lakini wanahitaji kupatiwa taaluma zaidi ili waweze kuendesha shughuli zao kwa uhakika.
“Soko letu ni zuri, lakini upatikanaji wa bidhaa yenyewe kidogo ina matatizo, na pia hatuna vifaa vya kutosha vya kisasa vya kuendeshea shughuli zetu” alisema  MAJID.
Bw. Majid amesema mradi huo unawasaidia vijana wengi wa Bweleo kupata ajira na wanasafirisha zaidi ya tan inane (8) kwa mwaka.
 
“Vijana 13 tumewaajiri katika mradi huu wa kamba na wavuvi zaidi ya 200 wanakuja kwenye mradi wetu kuuza kamba wao” alisema Majid ambaye pia anajishughulisha na ufugaji wa kuku.
Mapema akizungumza na vikundi vya wajasiriamali wanawake wa maeneo ya Bweleo vinavyojishughulisha na utengenezaji wa keki na vileja kwa kutumia mwani pamoja na mapambo kwa kutumia magamba ya chaza, Maalim Seif amesema Serikali inathamini juhudi zao za kujiletea maendeleo na kuahidi kushirikiana nao kuwaendeleza kitaaluma na kuwatafutia masoko.
 
Ameiagiza Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kufanya utafiti bei ya mwani katika soko la dunia ili kuwawezesha wakulima wa zao hilo kupata asilimia 80 ya bei ya soko hilo kama ilivyo kwa zao la karafuu.
Katika risala yao wanavikundi hao wameiomba serikali kufanya utaratibu wa kuwapatia eneo kwa ajili ya kujenga ofisi ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Nae Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Said Ali Mbarouk amesema vikundi vya wajasiria mali vya eneo la Bweleo ni vikundi vya mfano kwa kuendeleza mazao ya baharini, na kuahidi kushirikiana nao katika kuviendeleza.
 
Katika ziara hiyo Maalim Seif pia alitembelea ujenzi  wa Ofisi ya Mamlaka ya uvuvi wa Bahari kuu huko Fumba, ujenzi ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu na utagharimu dola za kimarikeni milioni mbili nukta nane 2.8 mln hadi kukamilika kwake.

No comments:

Post a Comment