Friday, October 21, 2011

USHAURI WA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF KWA UONGOZI WA KIWANDA CHA MATREKTA

PRESS RELEASE:

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameushauri uongozi wa Kiwanda cha kutengeneza Matrekta wa Jimbo la Sichuan Nchini Jamhuri ya Watu wa China Kufungua Tawi  lao Tanzania kwa lengo la kutoa huduma ndani ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Mashariki.

Balozi Seif Ametoa ushauri huo mara baada ya kukitembelea kiwanda hicho kilicho Wilaya ya Xindu katika Jimbo la Sichuan akiwa kwenye ziara ya kuangalia maeneo ya kiuchumi baada ya kuhudhuria Tamasha la Maonyesho ya Biashara na Viwanda Jimboni humo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameiwakilisha Tanzania katika Tamasha hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda.
Balozi Seif  alisema Hatua ya uwekaji Tawi hilo kwa kiasi kikubwa itazipunguzia gharama za uagizaji Nchi  za Ukanda wa Afrika Mashariki ambazi zinahitaji Matrekta kwa ajili ya kilimo.

“ Gharama za uagizaji wa bidhaa za Matrekta zinahitaji fedha nyingi kiasi ambacho ni mzigo kwa nchi zetu changa ambazo zinategemea zaidi kilimo ”. Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif alieleza kuwa Tanzania bado inategemea Kilimo katika kuimarisha uchumi wake. Hivyo mpango wake wa Kilimo kwanza unaweza kupiga hatua za haraka endapo kiwanda hicho kitafikia maamuzi ya kufungua Tawi lake Nchini Tanzania.

Alisisitiza kwamba mfumko wa bei kwa mwananchi wa kawaida unaweza kupungua au kuondoka kabisa ikiwa Sekta ya Kilimo itaimarishwa vilivyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameupongeza Uongozi wa Kiwanda hicho kwa mpango wake wa kutengeneza Matrekta yenye uwezo wa kuhudumia wakulima wa aina zote.

Naye Meneja mkuu wa Kiwanda cha utengenezaji wa Matrekta cha Jimbo la Sichuani Bw. Luo Zili amesema Kiwanda chao tayari kimeshafungua Masoko katika Mataifa ya Brazil, Sri Lanka, Laois na Zambia.
Bwana Luo Zili amefahamisha kwamba Uongozi wa Kiwanda  hicho umelenga  zaidi kutengeneza Matrekta na zana za Kilimo kwa Wakulima wadogo wadogo ili kuwapa nguvu za kuzalisha zaidi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.    21/10/2011.

No comments:

Post a Comment