Sunday, October 16, 2011

MKOANI YASHANGILIA KUPOKEA SHEREHE ZA MARIDHIANO

Wachezaji wa Ngoma ya Msewe wa Kambini wakionyesha umahiri wao wa kucheza ngoma hiyo.
Ngoma ya Tinge
Hadhira ya Mkoani

Na Aboud Mahmoud,Zanzibar
WILAYA ya Mkoani Kisiwani Pemba juzi ilirindima kutokana na burudani ya Ngona za asili zilizopagawisha wananchi wa Wilaya hiyo katika muendelezo wa tamasha la kusherehekea miaka miwili ya maridhiano.
Tamasha hilo lililofanyika katika uwanja wa ‘Umoja ni nguvu’ ambapo mamia ya wananchi hao wa kike na kiume walionekana kufurahia burudani zilizotolewa na wasanii wa ngoma za asilia.
Ngoma ya msewe wa Kambini-Kichokochwe ndio walioanza kutoa burudani hiyo ambayo iliondekana kuvuta hisia za mashabiki hao hasa pale walipokuwa wakiimba nyimbo zenye kutumia lahaja ya kisiwani hapo na kuchombeza kwa maneno ya kufurahia maridhiano.
Aidha wananchi waliojaa katika uwanja huo walishindwa kustahamili kukaa vitini na kuanza kuserebuka, ambapo kila mmoja alionekana kuguswa na midundo pamoja na maneno yaliotumika katika nyimbo hizo zilizoimbwa na kuchezwa na wenyewe wazee wenye asili ya ngoma hizo.
Aidha mara baada ya kumalizika kwa ngoma ya msewe,iliingia ngoma ya Tinge kutoka Tundauwa ilionekana kuwashangaza wengi kutokana na ustadi wa kucheza ngoma hiyo bila ya kutumia ala ya aina yoyote.
Ngoma hiyo ambayo inachezwa na wanaume watupu ambapo ngoma zake ni kupiga makofi na huchezwa kwa ustadi maalum wa uchezaji wake kwa kutumia miguu,ambapo nayo pia wananchi wa Mkoani ambao wengi wao ni mara ya kwanza kuiona ilivutia wananchi wengi huku wakiigiza jinsi wanavyoimba.
Baadhi ya maneno yaliokuwa yakitumika nyimbo zilizokuwa zikiimbwa kwenye ngoma ya Tinge ni pamoja na ‘Mbara mwezi dawa tuokote makarara’ na Tinge mkwajuni kwa Selemani kimeja’ ambapo hadhira iliyofika uwanjani hapo ilikuwa ikifatiza maneno hayo kutoka kwa wenyewe wachezaji wa ngoma hiyo.
Ufunguzi huo wa tamasha lililopewa jina la ‘Shangilia maridhiano’ kwa upande wa kisiwani Pemba,ulifunguliwa na Afisa tawala wa Wilaya ya Mkoani Abdullah Salim Abdullah,amewataka wananchi kutumia maridhiano hayo katika kuendeleza utamaduni wa ngoma za sili.
Amesema kuwa kufurahia maridhiano ni kuendeleza mshikamano kwa pamoja ni kuiletea maendeleo mengi Zanzibar,hivyo amewataka kudumisha maridhiano hayo pamoja na kuziendeleza ngoma za utamaduni.
Afisa Tawala huyo alianza yeye mwenyewe kutoa burudani kwa wananchi waliofika hapo kwa kuimba wimbo ‘Dawa dawa ,dawa dawa utamaduni ngoma za asili dawa, dawa!
Tamasha la 100% Zanzibari, Shangilia maridhiano lililoandaliwa na Kituo cha Sanaa za maonyesho za waswahili linatarajia kuendelea tena wiki ijayo katika kijiji cha Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja ambapo ngoma ya Mpe Chungu kutoka Makunduchi pamoja na kikundi cha Maendeleo (Profesa Gogo)kutoka Kangagani watatumbuiza siku hiyo.

No comments:

Post a Comment