Tuesday, October 25, 2011

 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
     Zanzibar                                                                                               25.10.2011
FINLAND imeeleza azma yake ya kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuendeleza Mradi wa  kutunza mazingira hapa Zanzibar (SMOLE).
 
Balozi wa Finland nchini Tanzania Mhe.Sinikka Antila aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungunzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
 
Katika mazungumzo hayo, balozi huyo wa Finland alimueleza Dk. Shein kuwa  Finland inathamini sana mashirikiano yaliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa nchi yake itahakikisha inaendelea kuunga mkono mradi wa SMOLE hapa Zanzibar.
 
Alisema kuwa   Finland ni nchi inayotajika na iliyopiga hatua kubwa katika masuala ya uhifadhi mazingira na misitu duniani hali ambayo ilisaidia kuinua uchumi wa nchi hiyo na  kueleza haja kwa Zanzibar ya kutunza mazingira kwani yanaweza kusaidia uchumi.
 
Balozi Antila alisema kuwa Finland imeanza kushirikiana na Zanzibar katika masuala ya uhifadhi mazingira na misitu kwa muda mrefu hivi sasa.
 
Alisema kuwa katika awamu ya pili ya mradi wa SMOLE ambao umeanza Julai 2010 hadi June 2013, nchi yake imetoa zaidi ya bilioni 8 katika kuhakikisha maendeleo ya mradi huo yanafikiwa.
 
Aidha, alieleza kuwa licha ya changamoto mbali mbali zikiwemo usajili wa ardhi, Balozi huyo alieleza kuwa anamatumaini makubwa ya mafanikio juu ya mradi huo na kusisitiza kuwa miongoni mwa madhumuni ya mradi huo ni kupambana na umasikini, kutunza mazingira na maendeleo ya kiuchumi.
 
Pamoja na hayo, balozi huyo alimueleza Mhe. Rais juu ya matarajio ya kuja Zanzibar Waziri anayeshughulikia masuala ya mazingira wa Nchi hiyo hapa Zanzibar hivi karibuni.
 
Nae Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Balozi huyo kutokana na ujio wake na kumueleza kuwa Finland ina historia kubwa katika mashirikiano na Zanzibar juu ya masuala ya mazingira na misitu.
 
Alieleza kuwa Finland imekuwa na mashirikiano mazuri na Zanzibar hatua ambayo imeweza kuisaidia Zanzibar katika masuala mazima ya mazingira sanjari na ujuzi ya masuala hayo.
 
Alisema kuwa Finland ni nchi ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa juu ya masuala ya mazingira hatua ambayo ilizipelekea nchi nyingi za Afrika kuja kufuata ujuzi hapa Zanzibar na kueleza kuwa kutokana na kuona umuhimu wa mazingira ndipo akachukua hatua za makusudi kuweka sekta hiyo chini ya Afisi ya Makamu wa Kwanza  wa Rais.
 
Dk. Shein pia, alimueleza balozi huyo kuwa kuna haja ya kuimatisha uhusiano kati ya Zanzibar na Finland katika sekta ya elimu, uhifadhi wa mazingira na mafunzo mengine muhimu juu ya mazingira na ardhi.
 
Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuitangaza zaidi Zanzibar nchini mwake katika medali ya Utalii pamoja na uwekezaji ambapo Balozi huyo wa Finland aliahidi kuifanya kazi hiyo ipasavyo.
 
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania anaemaliza muda wake wa kazi Mhe. Fatuma Ndangiza, Ikulu mjini Zanzibar.
 
Katika mazungumzo yao viongozi hao walieleza azma ya kushirikiano katika kuimarisha sekta za maendeleo kati ya Zanzibar na Rwanda ikiwemo sekta ya utalii, elimu ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na wakufunzi kwa vyuo vikuu vya SUZA na Kigali, utamaduni, mazingira na sekta nyenginezo.
 
Balozi Ndangiza alimpongeza Dk. Shein kwa mafanikio yaliopatikana Zanzibar kutokana na uchaguzi uliokuwa huru na haki na baadae kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni hatua ya kupigia mfano na kueleza matumaini yake ya kupatikana maendeleo endelevu hapa Zanzibar kutokana na uongozi imara wa Dk. Shein.
 
Mhe Ndangiza alimueleza Dk. Shein kuwa Rwanda imeona ipo haja ya kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya Utalii ambapo inatarajia kuanzisha safari za ndege kwa kutumia Shirika lake la ndege la nchi.
 
Katika mazungumzo hayo naye Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa hatua ya Shirika la ndege la nchi hiyo kutasaidia ushirikiano huo na kusisitiza Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Rwanda kwa manufaa ya nchi mbili hizo.
 
 Rajab Mkasaba

No comments:

Post a Comment