Friday, October 28, 2011

UTURUKI YAIPATIA TANZANIA MASHINE 10 ZA KUTUNZIA WATOTO WANAOZALIWA KABLA YA UMRI

Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dr.Sander Gurbuz (kushoto) akimkabidhi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr. Haji Mponda msaada wa mashine 10 za kutunzia watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda zenye thamani ya shilingi milioni 50 ambazo zitapelekwa katika hospitali mbalimbali nchini. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam. Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.

Na Bebi Kapenya- MAELEZO
Serikali imepokea msaada wa mashine maalum kumi kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania zenye thamani ya Tsh. Milioni 50 kwa lengo la kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla umri (watoto njiti) zitakazopelekwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo jijini Dar es Salaam Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt. Sander Gurbuz amesma kuwa nchi yake inathamini mchango wa Tanzania na hatua mbalimbali inazochukua katika kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa na wale walio chini ya umri wa miaka 5.

Amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya afya ili kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na kuiomba wizara hiyo kuzitunza mashine hizo ili ziendelelee kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu .

Balozi huyo amefafanua kuwa Serikali ya Uturuki imejikita katika kusaidia elimu na afya hususan utoaji wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wake Waziri Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda ameishukuru Serikali ya Uturuki kwa na kuahidi kuwa msaada huo utasaidia kuwahudumia watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri wao (watoto njiti) ambao hufariki kwa kukosa huduma hiyo.

Amefafanua kuwa katika nchi zinazoendelea karibu watoto milioni 10 walio chini ya miaka 5 hufariki kila mwaka huku asilimia 99 ya vifo hivyo ikitokea katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

“ Idadi ya vifo hivyo katika nchi zinazoendelea ni kubwa hivyo juhudi za makusudi zinahitajika katika kuondoa tatizo hilo, kwa upande wetu licha ya msaada tulioupata leo tunajitahidi kupunguza vifo vya watoto hao kwa kutumia mashine na wataalam waliopo katika hospitali mbalimbali nchini” Amesema.

No comments:

Post a Comment