Saturday, September 17, 2011

INDIA KUIPATIA ZANZIBAR TEKNOLOJIA YA KISASA YA KILIMO

 Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi zawadi ya mlango wa Zanzibar kwa Katibu Mkuu wa Jimbo la Andhra Pradesh Sutirtha Bhattacharya (katikati) mara baada ya kufanya mazungumzo mjini Hyderabad, India.
 
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitoa ufafanuzi kuhusu Zanzibar mbele ya katibu Mkuu wa Jimbo la Andhra Pradesh Sutirtha Bhattacharya (katikati) mara baada ya kufanya mazungumzo mjini Hyderabad, India. Katikati ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.

Hyderabad, India.
Serikai ya jimbo la Andhra Pradesh nchini India imesema iko tayari kuipatia Zanzibar teknolojia ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji pamoja na kuiongezea nguvu za kuimarisha miundo mbinu ya kiuchumi kama njia ya kusaidia juhudi za kukuza maendeleo na kuinua hali za wananchi wa Zanzibar.
Ahadi hiyo imetolewa Katibu Mkuu wa jimbo hilo, Sutritha Bhattacharya alipokuwa na mazungumzo na Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad katika kikao kilichoifanyika katika ofisi za jimbo hilo mjini Hyderabad India.
Katibu huyo akiwa pamoja na viongozi wa jimbo hilo amesema ni jambo lililowazi India imeweza kupiga hatua kubwa katika kilimo baada ya kuimarisha miundo mbinu yake na kuweka mkazo katika kilimo cha kisasa hasa mpunga na matokeo yake imekuwa miongoni mwa wasafirishaji wakuu wa zao hilo duniani.
Alimueleza Makamo wa Kwanza wa Rais kuwa India iko tayari kutoa mbinu hizo kwa Zanzibar na haitasita kuwapeleka wataalamu wake Zanzibar, iwapo serikali hiyo itaona haja ya kufanywa hivyo.
“Tuko tayari kuleta wataalamu wetu Zanzibar watoe mbinu tunazozitumia ambazo bila ya shaka yoyote zimetusaidia kupiga hatua na kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uzalishaji wa mpunga duniani”, alisema Katibu wa jimbo hilo.
Alisema kwamba Zanzibar inaweza kujifunza taratibu za Andhra Pradesh katika shughuli za kiuchumi ambapo sekta za watu binafsi zinapata mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mkubwa kati yake na serikali.
Alieleza kwamba kilimo pamoja na biashara ndogo ndogo na za kati vimepewa umuhimu wa kipekee na jimbo hilo pamoja na serikali kuu ya India, na kwamba India tokea ilipoingia katika sera za biashara huria mwaka 1991 wananchi wamepata matumaini makubwa na maeneo mengi yameonesha mafanikio.
Bhattacharya amesema siri ya maendeleo yanayopatikana katika jimbo hilo ni kutekelezwa sera ya ushirikiano kati ya makampuni ya watu binafsi na taasisi za serikali na hata pale watu binafsi wanapokumbwa na matatizo serikali inakuwa mstari wa mbele kuwafidia kwa nia ya kuwawezesha kuendelea na shughuli zao.
“Mmekuja mahala penyewe hasa, Andhra ndio makao makuu ya kampuni nyingi za uzalishaji India, lakini kwa upande mwengine kumepata sifa ya kipekee ya kuwa wazalishaji wakuu wa mpunga kwa ajili ya biashara na matumizi ya ndani, matumaini yetu baada ya mazungumzo mtaanisha maeneo gani mtaweza kunufaika na teknolojia tuliyonayo”, alisema Katibu huyo.
Aidha, alisema chuo kikuu cha Kilimo cha Acharian Agricultural University ambacho ndio chanzo cha mafanikio ya kilimo India kipo katika jimbo hilo na Zanzibar inaweza kunufaika na utaalamu wa kilimo na usindikaji wa bidhaa unaotolewa na chuo hicho.
Katika mazungumzo hayo, Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad amesema India ni rafiki wa muda mrefu wa Zanzibar na Tanznaia kwa ujumla na kwamba kuna fursa kubwa kwa makampuni ya nchini hiyo kutumia fursa hiyo kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande mbili hizo.
Alisema India iko mstari wa mbele katika nyanja tafauti za kiuchumi na imeweza kujipatia sifa kubwa katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo kwa ujumla.
Maalim Seif alisema amefarajika kufuatia mazungumzo hayo na serikali ya Zanzibar itakaa ili kuona ni maeneo gani yanayoweza kutekelezwa na kunufaika na utaalamu wa Andhra Pradesh katika Nyanja tafauti kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban alisema Zanzibar inaweza kunufaika na teknolojia na utaalamu wa kuendesha viwanda vidogo vidogo kutoka India, kama ambavyo nchi hiyo ilivyoisaidia Zanzibar wakati wa awamu ya pili ya uongozi, ambapo viwanda vingi vidogo vidogo viliweza kufunguliwa.
Maeneo mengine ambayo jimbo hilo limepata mafanikio makubw akatika kuimarisgha miundoi mbinu yake ni sekta za utalii, bandari na viwanja vya ndege, miundo mbinu ya barabara,reli pamoja na uhifadhi wa bidhaa.
Makamo Mwenyekiti wa Kampuni ya Miundo mbinu ya Andhra Pradesh, Yusuf Ali alisema Zanzibar inaweza kupata mafanikio makubwa katika sekta hizo za kiuchumi, iwapo itafanya utafiti na kuimarisha miundo mbinu yake ya kiuchumi.
Zanzibar imeweka mkazo mkubwa kuimarisha kilimo cha kisasa cha umwagiliaji, kupitia mkakati wake wa Mapinduzi ya kilimo nia ikiwa ni kuwa na uhakika wa chakula na kupunguza utegemezi wa bidhaa zenye mahitaji ya kila siku. 
Imetumwa na Hassan Hamad kutoka (OMKR)
Mhariri: Ali Mohammed 

No comments:

Post a Comment