Thursday, July 26, 2012

MELI TATU ZAFUTIWA HATI YA KUFANYA KAZI ZANZIBAR.


Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo

Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi hati ya kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na meli hizo kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika meli hizo.

Aidha meli hizo zimepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama Zanzibar.
Amesema Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha na kujiridhisha kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar jambo ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli hizo.

Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka kufanya maamuzi hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu na kupata matatizo mara kwa mara katika safari zao.

Kombo amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri na Bandari Zanzibar ya mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.

Kufuatia sheria hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa Meli hizo kuzirudisha hati za kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta sehemu nyengine za usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar.

Akizungumzia Meli ya Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo kupunguza idadi ya abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani za mizigo kutoka 100 hadi 50  hadi pale ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo.

Aidha amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa italeta Meli kubwa ya abiria itakayofanya kazi zake Zanzibar ambapo pia Serikali ya Mapinduzi nayo iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.


Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
26/07/2012

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR NA VIKOSI VYA ULINZI PAMOJA NA TAASISI ZA KIRAIA WAPONGEZWA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mkuu wa Mabalozi wa Nchi za Nje waliopo Tanzania Bwana Juma Alfan Mipango hapo Ofisini kwake Baraza la wawakilishi Mbweni.
Pembani yao ni Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu { UAE } Bw.Mallallah  Mubarak Alameri.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  akizungumza na Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Pencheni wa PPF Bibi Lulu Mengele aliyefika Zanzibar kutoa mkono wa pole kwa niaba ya Uongozi wa Mfuko huo kufuatia ajali ya meli ya hivi karibuni karibu na Kisiwa cha chumbe Zanzibar.

Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Pencheni { PPF } Bibi Lulu Mengele akiwasilisha salamu za rambi rambi kwa Makamu wa PILI WA Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kufuatia ajali ya Meli ya M.V.Skagit iliyotokea wiki iliyopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Bishop Michael wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar mara baada ya kuwasilisha salamu zao za rambi rambi hapo ukumbi wa Baraza la wawakilishi Mbweni.
Pembeni ni Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo Bwana Nuhu Sallanya.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano na Vikosi vya Ulinzi, pamoja na Taasisi za Kiraia imepongezwa kwa hatua  iliyochukuwa  katika kukabiliana na Maafa yaliyotokea ya kuzama kwa Meli ya M.V. Skagit wiki iliyopita.
Pongezi hizo zimetolewa na Uongozi wa Taasisi tofauti zinazoendelea kutoa mkono wa pole  hapa Zanzibar kufuatia vifo vya watu kadhaa waliokuwemo ndani ya Meli hiyo iliyopata ajali karibu na Kisiwa cha Chumbe.
Afisa Uhusiano wa Mfuko wa Pencheni { PPF } Bibi Lulu Mengele Bishop  Michael wa Kanisa la Anglicana Dayosisi ya Zanzibar pamoja na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu { UAE } Bwana Mallallah Mubarak Alameri wakitoa mkono huo wa pole kwa Balozi Seif walisema hatua hiyo imesaidia kuokoa maisha ya wananchi kadhaa.
Walisema walio wengi wameshuhudia jitihada hizo za uokozi zilizoleta matumaini ndani ya nyoyo za Jamii.

Hata hivyo wawakilishi hao wa taaasisi tofauti walisema licha ya juhudi hizo za Serikali lakini bado ipo haja ya msingi ya kufuatwa kwa sheria na Taratibu sa usafiri wa Baharini.
Walisema utaratibu huo mbali ya kupunguza zinazoweza kuepukwa lakini pia utasaidia kuondosha mwanya kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji wakorofi wanaoendesha biashara hiyo ya vyombo vya usafiri wa Baharini.
“ Kitu cha msingi ni kufuatwa kwa sheria na taratibu za usafiri nah ii itaondosha uzembe na ujanja unaotumiwa na wafanyabiashara wakorofi”. Alisisitiza Balozi wa UAE Bwana Mallallah.

Naye kwa upande wake Bishop Michael wa Kanisa la Anglikana la Mkunazini Dayosisi ya Zanzibar amesema hatua za serikali za kurejesha hali ya amani kufuatia fujo za  baadhi ya Vijana zilizofanywa hivi karibuni imeleta faraja kwa waumini wa kanila lao.
Bishop Michael alisema Uongozi wa Kanisa hilo utaendelea kuwaelimisha Waumini wao kulinda na kuheshimu amani ya Taifa ambayo inahitajiwa na kila mwana Jamii.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi wa Serikali wanaendelea kupata matumaini kuona Taasisi na mshirika mbali mbali ndani na nje ya Nchi yanaunga mkono juhudi za Serikali.
Balozi Seif alisema Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukuwa hatua madhubuti ili kuzuia majanga yanayoweza kuwepukwa ambayo yamo ndani ya uwezo wa mwanaadamu.
“ Tumeanza kuchukuwa hatua za kukabiliana na hali hii kwa kuwaomba washirika wetu ndani na nje ya Nchi kutusaidia katika sekta hii Likiwemo hili zito la upatikanaji wa meli kubwa ya usafirishaji wa wabiria na mizigo”. Alifafanua Balozi Seif.

 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/7/2012.