Monday, October 31, 2011

JUMUIYA YA TEKNOLOJIA YA AFYA KULETA WATAALAMU ZANZIBAR

Washington DC:-
 
Jumuiya inayojishughulisha na Teknolojia ya Afya { MED } Nchini marekani inajipanga kuandaa ratiba ya Wataalamu wao wa afya kuja Zanzibar kusaidia huduma za afya katika Hospitali za Visiwani.
Mwakilishi wa jumuiya hiyo kutoka chuo Kikuu cha Brown Nchini Marekani Bwana jayson Marwaha ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Ubalozi wa Tanzania Mjini Washington DC.
 
Bw. Jayson alisema Jumuiya yake imeshatenga kiasi cha Dolla za Kimarekani 14,000 kwa ajili ya kusaidia huduma za afya katika Vituo vya Afya vilivyomo vijijini kupitia shirika la misaada la Marekani US aid.
 
Bw. Jayson alimueleza Balozi Seif kwamba mpango huo utakaojumuisha huduma za  uchunguzi wa Virusi vya Ukimwi, huduma za watoto pamoja na mafunzo ya matumizi ya Vifaa vya kisasa utaanzia nchini Malawi.
Mwakilishi huyo wa MED alisema kwamba Taasisi yake itaendelea kuangalia maeneo ambayo inaweza ikaisaidia Zanzibar katika masuala ya Afya.
 
Mapema Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mamboya alimueleza Mwakilishi huyo wa Jumuiya inayojishughulishs na Teknolojia ya Afya kwamba Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa katika huduma za akina mama na watoto.Dr. Sira amesema kinachozingatiwa zaidi hivi sasa na serikali ni mipango ya kuziwezesha Hospitali za Mikoa kutoa huduma za lazima za afya ili kupunguza wimbi la wagonjwa katika Hospitali Kuu ya Manazi Mmoja.
 
Akitoa shukrani zake Mkamu wa Pili wa Ris wa Zanzibar balozi Seif Ameipongeza Taasisi hiyo kwa  juhudi zake za kuonyesha moyo wa kusaidia sekta ya afya Zanzibar.
Balozi Seif alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na baadhi ya wataalamu wanaosaidia huduma za afya kutoka mashirika na nchi wahisani..
 
"Tumekuwa tukipokea Madaktari wa fani tofauti kutoka China na Cuba. Sasa kuwepo kwenu Zanzibar na nyinyi Mtasaidia kuongeza huduma za Afya kwa Wananchi walio wengi ". Alisema Balozi Seif.
 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
30/10/2011.

Friday, October 28, 2011

TATIZO LA UHARAMIA KATIKA BAHARI YA AFRIKA MASHARIKI LINALETA ATHARI KUBWA ZA KIUCHUMI - MAALIM SEIF

Maalim Seif akiagana na Waziri wa Maendeleo wa Finland Bibi Heidi Hautala baada ya kumaliza mazungumzo ofisini kwake Migombani
Maalim Seif akizungumza na Waziri wa Maendeleo wa Finland Bibi Heidi Hautala Ofisini kwake Migombani Mjini Zanzibar (Picha: Salmin Said-OMKR)

Na: Hassan Hamad (OMKR).

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema tatizo la uharamia katika bahari ya Afrika Mashariki linaleta athari kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema wafanyabiashara wamekuwa wakizungunguka masafa marefu kuwakimbia maharamia, jambo ambalo linapelekea kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na kuleta malalamiko kwa wananchi kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa mbali mbali zikiwemo za vyakula.
Maalim Seif ameeleza hayo huko Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na Waziri wa Maendeleo wa Finland bibi Heidi Hautala.
Ameiomba jamii ya kimataifa kuangalia uwezekano wa kulidhibiti suala hilo ili kuleta unafuu kwa wafanyabiashara na hatimae wananchi waweze kunufaika kwa kuweza kumudu bei za bidhaa hasa vyakula.
Amesema suala hilo linaweza kudhibitiwa iwapo jamii ya kimataifa itaweka mikakati imara ikiwa ni pamoja na kushirikiana na viongozi wa mataifa yanayokumbwa na tatizo hilo.
Akizungumzia kuhusu mazingira Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kuhifadhi rasilimali asilia zikiwemo misitu na vianzio vya maji ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa matumizi mbali mbali.
Amesema tatizo la uharibifu wa mazingira limekuwa likileta athari kubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kukosekana mvua kwa wakati pamoja na upungufu wa maji safi na salama kutokana na vianzio vyake kuharibiwa.
Kwa upande mwengine Maalim Seif amesema serikali inajipanga kusimamia udhibiti wa ardhi, ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 asilimia 50 ya ardhi iwe imesajiliwa, na kwamba hatua hiyo itasaidia kuweka mipango imara ya kutenganisha maeneo ya kilimo na yale ya makaazi.
Amefahamisha kuwa Serikali pia inazihamasisha taasisi za kijamii na zile za binafsi kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira ili jamii nayo ipate mwamko wa kutosha juu ya umuhimu wa kuyalinda mazingira yao.
Kuhusu dawa za kulevya, Maalim Seif amesema serikali inaendelea na mkakati wake wa kuwaunganisha vijana walioathirika na utumiaji wa dawa za kulevya kwa lengo la kuwasaidia kupata ajira, ili waweze kuepukana na kujishughulisha na dawa hizo.
Amesema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watu wanaojihusisha na dawa za kulevya ambapo kupitia Wizara ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi vijana wanahamasishwa kujiunga na vikundi vya ushirika ili wawezeshwe kujikwamua kiuchumi.
Amebainisha kuwa utumiaji wa dawa za kulevya unaongeza umaskini katika ngazi ya familia hadi taifa, kwa vile watumiaji hao wakati mwengine huiba vitu vya nyumbani na kuviuza kwa bei nafuu kwa dhamira ya kujitafutia mahiji yao, jambo ambalo hurejesha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo.
Nae Waziri wa biashara wa Finland bibi Heidi Hautala amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya kwani zimekuwa zikichangia uhalifu katika nchi mbali mbali.
Amesema iwapo vijana watawezeshwa kiuchumi na kupewa elimu ya kutosha juu ya janga hilo wanaweze kuachana na vitendo hivyo na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kuhusu Mazingira Waziri huyo amesema ipo haja kwa Zanzibar kuzingatia umuhimu wa matumizi bora ya Ardhi, kwani iwapo itatumika ipasavyo itasaidia harakati za maendeleo na kiuchumi kwa urahisi zaidi.
Bibi Hautala ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Finland na Zanzibar, sambamba na kuiendeleza miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na nchi hiyo  ukiwemo mradi wa uhifadhi wa ardhi na mazingira wa SMOLE.

UTURUKI YAIPATIA TANZANIA MASHINE 10 ZA KUTUNZIA WATOTO WANAOZALIWA KABLA YA UMRI

Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dr.Sander Gurbuz (kushoto) akimkabidhi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr. Haji Mponda msaada wa mashine 10 za kutunzia watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda zenye thamani ya shilingi milioni 50 ambazo zitapelekwa katika hospitali mbalimbali nchini. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam. Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.

Na Bebi Kapenya- MAELEZO
Serikali imepokea msaada wa mashine maalum kumi kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania zenye thamani ya Tsh. Milioni 50 kwa lengo la kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla umri (watoto njiti) zitakazopelekwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo jijini Dar es Salaam Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt. Sander Gurbuz amesma kuwa nchi yake inathamini mchango wa Tanzania na hatua mbalimbali inazochukua katika kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa na wale walio chini ya umri wa miaka 5.

Amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya afya ili kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na kuiomba wizara hiyo kuzitunza mashine hizo ili ziendelelee kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu .

Balozi huyo amefafanua kuwa Serikali ya Uturuki imejikita katika kusaidia elimu na afya hususan utoaji wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wake Waziri Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda ameishukuru Serikali ya Uturuki kwa na kuahidi kuwa msaada huo utasaidia kuwahudumia watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri wao (watoto njiti) ambao hufariki kwa kukosa huduma hiyo.

Amefafanua kuwa katika nchi zinazoendelea karibu watoto milioni 10 walio chini ya miaka 5 hufariki kila mwaka huku asilimia 99 ya vifo hivyo ikitokea katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

“ Idadi ya vifo hivyo katika nchi zinazoendelea ni kubwa hivyo juhudi za makusudi zinahitajika katika kuondoa tatizo hilo, kwa upande wetu licha ya msaada tulioupata leo tunajitahidi kupunguza vifo vya watoto hao kwa kutumia mashine na wataalam waliopo katika hospitali mbalimbali nchini” Amesema.

MWANAHABARI WA RADIO FREE AFRIKA NA STAR TV IRINGA ANUSURIKA KUUWAWA

Frederick Siwale

Na Francis Godwin Blog,Iringa
MWANDISHI wa habari wa Radio Free Afrika na Star Tv mkoa wa Iringa Frederick Siwale(49) (pichani) amenusurika kuuwawa na viongozi wa serikali ya kijiji cha Maleusi wilaya ya Makete mkoani Iringa baada ya kuwekewa magogo njiani kwa lengo la kumteka na kumfanyia unyama huo alipokuwa akifuatilia sakata ya mgogoro wa ardhi kijijini hapo.

Tayari jeshi la polisi mkoani Iringa linawashikilia viongozi wawili wa serikali ya kijiji cha Maleusi katika Wilaya ya Makete mkoani Iringa kwa tuhuma za kutaka kumfanyia unyama huo mwanahabari huyo .

Siwale alikutwa na mkasa huo majira ya saa tano asubuhi baada ya kufika kijijni hapo kwa ajili ya kufuatilia na kuripoti sakata ya mgogoro wa ardhi uliozuka kati ya pande mbili kati ya kijiji na familia .

Kiini cha tukio hilo kimefahamika kuwa ni viongozi hao kuhusishwa katika tuhuma za ubadhilifu wa ardhi iliyotumika kwa maziko ya wananchi kuibinafsisha kwa mwekezaji.

Eneo lilitumika kwa maziko ambalo limefahamika kuwa nila ukoo wa Mbilinyi ambao kwa mujibu wa wasemaji wa ukoo huo Nazarena Mbilinyi na Paulo Mbilinyi eneo hilo lilianza kutumika kwa maziko tangu mwaka 1945.

Akizungumzia tukio hilo Siwale alisema baada ya kupata taarifa ya kuuzwa kwa eneo la makaburi kama ilivyo ada ya kazi yake alifunga safari kwenda Makete ili kupata undani wa tukio hilo.

“Nilifika Makete na siku iliyofuata nilianza safari ya kwenda kijijini huko Maleusi kwa ajili ya kukamilisha kazi yangu ya kihabari, nilipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi ikiwa pamoja na wahusika wa ukoo wa Mbilinyi waliokuwa wakiwalalamikia viongozi hao, lakini nilipotaka kukamilisha habari yangu kwa walalamikiwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji aliwaita wajumbe na kuamuru ngoma ya lamgambo na mtendaji alipiga simu ambayo alisikika akisema njiani yawekwe magogo ili kunizuia kupita, na niliposikia hivyo nilikimbia kwa kubadili njia ndiyo ilikuwa salama yangu,” Alisema Siwale.

Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Iringa Evarist Mangala alikiri kukamatwa kwa viongozi hao ambao aliwataja majina watuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Rubern Mbilinyi mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Maleusi na Michael Sanga ambaye ni afisa mtendaji wa kijiji cha maleusi na kuwa watafikishwa mahakani baada ya uchunguzi kukamilika.


Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) imeeleza kusikitishwa na hatua ya viongozi hao wa vijiji kutaka kwenda kinyume na katiba ya nchi ambayo inatoa nafasi kwa kila mtanzani kupata habari na ile ya uhuru wa vyombo vya habari inayowataka wanahabari kufanya kazi yao bila kunyanyaswa.

Katibu mtendaji wa IPC Frank Leonrad alisema kuwa mbali ya kulipongeza jeshi la polisi mkoa wa Iringa kupitia kamanda wake Mangalla kwa kuwakamata wahusika hao bado alitaka viongozi wa serikali kutowaona wanahabari wanaofika katika maeneo yao kuwa ni maadui .

U.S. EMBASSY HOSTS SECOND SEMINAR ON INFORMATION TECHNOLOGY

he U.S. Embassy in Dar es Salaam hosted the second of a series of seminars for Information Technology (IT) professionals in Tanzania on October 28. Over 45 guests from Dar es Salaam, Arusha, and Zanzibar attended to share their experiences and ideas for using technology to improve IT operations in businesses and government offices. The theme for this year's seminar was "Security and Costs Saving."


The U.S. Embassy in Dar es Salaam hosted the second of a series of seminars for Information Technology (IT) professionals in Tanzania on October 28. Over 45 guests from Dar es Salaam, Arusha, and Zanzibar attended to share their experiences and ideas for using technology to improve IT operations in businesses and government offices. The theme for this year's seminar was "Security and Cost Saving."
With the fast pace of IT industry and the unique challenges of operating in Dar es Salaam, the opportunity to exchange ideas assists Tanzanian managers and IT administrators adapt to a constantly-changing environment and implement technologies that lead to cost savings and preserving the environment. This second seminar featured presentations by U.S. Embassy speakers titled "Social Media & Security," "Green the New Color in IT," and "Working Across Cultures."
Senior Embassy Systems Administrator Sajjad Gulamali said, "We hope these presentations start a conversation between a variety of businesses and government officials about how to use technology to make information easier to access, share, use and lead to cost saving." Embassy Assistant Senior Manager for IT Murtaza H Lalji discussed green waste disposal procedures as a tool to protect the environment and enhance IT operations.
Embassy Information Management Officer Walter Cunningham explained that the seminar series intended to facilitate information exchange: "We wanted to establish a forum in Tanzania by sharing some of the things that work for us in the U.S. Department of State and seek better ways of accomplishing our IT goals in partnership with Tanzanian professionals. We look forward to our continued partnership with this key sector which is leading Tanzania's growth in the information field."

The program featured a presentation on virtualization by Mr. Ali Thawer, one of the founders of Bell Communications Ltd who presently serves as a CEO. Mr. Thawer recently visited the United States of America under the International Visitors Leadership Program (IVLP) "A New Beginning: Entrepreneurship and Business Innovation." In his remarks, he discussed virtualization and his visit to the U.S., where he established professional ongoing contacts with 30 colleagues from other nations.
Guest of honor Ms. Elizabeth Mzagi, Acting Director of the Tanzania Communications Regulatory authority, told the audience that the Government of Tanzania is currently developing policy on green waste to protect the environment. The first seminar for IT professionals was held on December 4, 2009. The U.S. Embassy hopes to organize future regular forums and welcomes presentation submissions from Tanzanian colleagues in the IT field. For additional information about upcoming IT Seminars, or to submit presentation ideas for review, please send an email to usembassydar@gmail.com.

WIZARA YA NISHATI YASAINI MKATABA WA DOLA MILIONI 70 NA MAKAMPUNI YA MAFUTA

Na Ismail Ngayonga - MAELEZO, Dar es Salaam
WIZARA ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wamewekeana saini ya mkataba na makampuni ya Ndovu resource na Heritage Oil kutoka nchini Uingereza kwa ajili ya uchimbaji na utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi katika Kisiwa cha Songosongo na Ziwa Rukwa.

Akizungumza katika hafla hiyo jana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema uwekaji saini wa mikataba na makampuni hayo unaifanya Tanzania kuwa na mikataba 23 na makampuni 17 ya utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Alizitaja nchi zenye makampuni hayo ni Australia, Uingereza, Ufaransa, Brazil, Norway, Marekani, Canada na Nchi za Falme ya Kiarabu.

Waziri Ngeleja alisema utiaji saini na makampuni hayo ni kielelezo cha sera nzuri zilizopo katika sekta ya nishati na hivyo kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kivutio cha uwekezaji kwa kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

“Mikataba hii imezingatia maslahi ya taifa pamoja na makampuni haya kufuata sheria za nchi yetu ikiwemo suala zima la uhifadhi wa mazingira ambalo ni jambo la msingi kwa wananchi wetu” alisema Ngeleja. 
 
Aidha Waziri Ngeleja aliitaka TODC kusimamia vyema masharti ya mikataba hiyo ikiwemo fedha zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo ya watumishi wa shirika hilo yanayolenga kuliwezesha taifa kupata wataalamu wake wataosimamia vyema rasilimali za mafuta na gesi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Yona Killagane alisema ujio wa makampuni hayo ni fursa nzuri iliyopata Tanzania katika kufumbua vyanzo mbalimbali vya nishati ya mafuta na gesi vilivyopo nchini.
“Kabla ya kufikia hatua hii ya utiaji saini, tulichukua hatua za makusudi ili kujiridhisha kuwa mikataba hii itazingatia maslahi ya taifa” alisema Killagane.
 
Naye Kamishina Msaidizi wa maendeleo ya gesi na petrol katika Wizara ya Nishati na Madini, Prosper Victus alisema mikataba hiyo itagharimu kiasi cha Dola Milioni 70 na shughuli hiyo ya utafutaji wa nishati hizo za inatarajia kuchukua kipindi cha miaka 11 iliyogawanywa katika awamu 3 za utekelezaji.
 
Alisema kampuni ya Ndovu Resource itachimba nishati hiyo ya mafuta na gesi katika eneo la songosongo mashariki wakati kampuni ya Heritage Oil itafanya shughuli hiyo katika ziwa Rukwa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Ndovu Resource, Brian Hall alisema kampuni yake itaheshimu vipengele vya mkataba huo ikiwemo suala la uchangiaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya uchimbaji wa nishati hizo.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kampuni ya heritage Oil, Brian Smith alisema kampuni yake itahakikisha suala la ajira kwa vijana linapewa kipaumbele, kwani nia ya taasisi hiyo ni kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya umaskini kwa wananchi wake.

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI ANAONDOKA LEO KUELEKEA MAREKANI KIKAZI KWA SIKU KUMI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka  Nchini leo kwa safari ya Kikazi ya siku kumi  Nchini Marekani.  

Balozi  Seif aliyepata mualiko kutoka kwa shirika la uwekezaji vitega uchumi Afrika la Nchini Marekani anauongoza Ujumbe wa  Viongozi Sita  wa Kiserikali akiwemo Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi. 

Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  inalenga   Zanzibar kujitangaza zaidi Nchini Marekani katika Uwekezaji kwenye maeneo yaliyomo ndani ya Sekta za  Utalii, Biashara, Elimu, Kilimo, Afya, Miundo Mbinu pamoja  na Mazingira.

Viongozi anaofuatana nao katika Ziara hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha ,Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mh. Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Fatma Alhabib Fereji na Naibu Waziri wa Afya Dr. Sira Ubwa Mamboya.

Wengine ni Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Mh. Salmin Awadh Salmin, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Nd. Julian Raphael, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis Nassor wakiwemo pia  baadhi ya Wafanya biashara.

Balozi Seif na Ujumbe wake ataanza Ziara yake kwa kukutana na Uongozi wa Taasisi ya Biashara na Maendeleo { USTDA } pamoja na Mwakilishi wa  Taasisi ya Biashara na Vitega Uchumi inayosimamia Sera ya Biashara { USTR }.

Pia atakutana na Uongozi wa Shirika la Uwekezaji Vitega Uchumi
{ OPIG } linalofadhili Miradi ya Biashara ambapo siku inayofuata  atakaguwa Bandari ya  kwanza kwa upokeaji kwa wingi Bidhaa kutoka nje  ya Maarekani ya Houston kwenye Ghuba ya Mexico pamoja na kukutana na Washirika wa masuala ya Biashara Mjini Houston.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake ataendelea na ziara yake katika Mji wa Florida kwa kukitembelea Chuo Kikuu cha Kilimo na Ufundi cha Florida { FAMU }.

Balozi Seif anatarajiwa kuondoka Washington Nchini Marekani Tarehe 6 Oktoba 2011 na kurejea nyumbani akiuacha Ujumbe wake kuendelea na ziara ya siku tatu ya kukutana na Viongozi wa Taasisi mbali mbali za Uwekezaji Nchini humo ukiwemo Uongozi wa Benki Mashuhuri Duniani ya Exim Bank.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/10/2011.

Tuesday, October 25, 2011

MAALIM SEIF ASEMA SERIKALI INATOA UMUHIMU WA KIPEKEE KULINDA ARDHI YA VISIWA VYA UNGUJA NA PEMBA

Balozi wa Finland nchini Tanzania SINIKKA ANTILA akizungumza na Maalim Seif alipofika Ofisini kwake Migombani kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali hasa yanayohusu mazingira.
Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej akizungumza na Balozi wa Finland nchini Tanzania SINIKKA ANTILA Ofisini kwake Migombani. (Picha Salmin Said-OMKR)

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali inatoa umuhimu wa kipekee kuilinda ardhi na mazingira ya visiwa vya Unguja na Pemba yasiharibiwe na matendo ya binadamu na athari za majanga ya kimaumbile.

Maalim Seif ameeleza hay oleo alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Finland nchini Tanzania Bibi Sinikka Antila alipofanya mazungumzo nae huko Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.

Amesema miongoni mwa changamoto zinazotaka zipatiwe ufumbuzi wa haraka na serikali ni ongezeko la watu katika maeneo ya mijini, ukataji miti ovyo pamoja na baadhi ya wananchi kufanya ujenzi katika maeneo yasiyoruhusiwa yakiwemo ya kilimo na maeneo ya wazi.

Makamu wa kwanza wa Rais amesema juhudi kubwa zinachukuliwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi hasa kwa vile nchi za visiwa kama Zanzibar yenye ardhi ndogo, inaweza kukosa ardhi kwa matumizi ya mambo ya maendeleo na kijamii.

“Matumizi ya ardhi ni suala linalotuumiza vichwa sana, baadhi ya watu wana tabia ya kujenga kwenye maeneo yenye rutba yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo, maeneo ya wazi na tunakabiliana na tatizo la ukataji miti ovyo hata kwenye vyanzo vya maji”, amesema Maalim Seif Seif.

Pia Maalim Seif ameelezea mkakati wa kupanda miti katika maeneo yaliyoathiriwa na uchafuzi wa mazingira hasa katika kisiwa cha Pemba, ili kujikinga na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameanza kujitokeza.

Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania Bibi Sinikka Antila amesema nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika suala la uhifadhi wa mazingira.

Amesema mazingira ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, hivyo hayana budi kulindwa na kuhifadhiwa kwa nguvu zote ikiwa ni pamoja na kupanda miti.

“Nchini kwetu kuna kanuni isemayo, ‘kata mti mmoja panda miwili’”, alisema balozi Sinikka.

Finland ni miongoni mwa nchi zinazotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar hasa katika masuala ya mazingira ambapo kwa sasa inasimamia mradi mkubwa wa usimamizi wa ardhi na mazingira Zanzibar (SMOLE).

MAKAMU WA RAIS AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA KIMATAIFA WA MAWASILIANO (ITU) JIJINI GENEVA, SWITZERLAND OKTOBA 25, 2011

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Tanzania Youth Alliance (TAYOA), Peter Masika, kuhusu namna ya kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta, wakati akikagua banda la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Tanzania Youth Alliance (TAYOA), Peter Masika, wakati akitazama mashine ya mawasiliano (ICT Mobile Booth), iliyotengenezwa na vijana wa TAYOA, wakati akikagua banda la maonyesho la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiangalia mfumo wa kuwasiliana kwa masafa (tele-conference) katika Banda la HUWAWEI, wakati akitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika maonyesho ya ITU, jijini Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011. Picha na Muhidin Sufiani-OMR

Na Boniphace Makene
MHMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa ITU (International Telecommunication Union) unaohusu wajibu nchi katika dhana ya mawasiliano unaofanyika jijini Geneva.
Makamu wa Rais ambaye ameambatana na wadau wa masuala ya mawasiliano kutoka Tanzania, sambamba na kushiriki kutoa mada katika mjadala unaohusu ‘Utandawazi na Dunia kuwa kijiji’ mjadala ambao pia umewashirikisha Balozi Philip Verveer wa Marekani, Waziri Mkuu wa Rwanda, David Kanamugire, Naibu Waziri Mkuu wa Bahrain, Shaikh Ali Bin Khalifa Al Khalifa,
Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal Alassane Dialy Ndiaye na kusimamiwa na Mtangazaji wa CNN, Becky Anderson, ametumia fursa hiyo kuuelezea ulimwengu juu ya fursa zinazotokana na Tanzania kuwekeza katika mkongo wa intaneti chini ya bahari ya Hindi ambao kwa kiwango kikubwa umetanua urahisi wa mawasiliano kati ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kusini.
Kupitia mkongo huo, nchi jirani zitarahisisha mawasiliano yake ya Intaneti kupitia Tanzania na taifa litanufaika na gharama za malipo kutoka katika nchi hizo. Malawi ni moja ya nchi ambazo tayari zimeonyesha nia ya kutaka kuunganishwa haraka.
Makamu wa Rais pia amezungumzia ukuaji wa mtandao wa simu ambapo sasa Tanzania kuna kadi za simu milioni 12 ambazo zimesajiliwa na kufafanua kuwa licha ya kuwa idadi inaongezeka katika matumizi ya teknolojia, bado upo uwanda ambao haujatumika hivyo wawekezaji wanakaribishwa sana kuwekeza huku wakifahamu Tanzania ni nchi ya amani na yenye fursa nyingi sambamba na kuwa na watu walio wepesi wa kupokea mabadiliko.
Tanzania inalo banda la maonyesho hapa katika uwanja kunakofanyika mkutano huu wa ITU, banda ambalo linasimamiwa na TCRA, sambamba na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya ambao wanelezea namna Tanzania inavyoweza kutoa huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya ICT, wahamasishaji vijana kuhusu ugonjwa wa Ukimwi TAYOA na UhuruOne ambao wanajihusisha na utoaji huduma za kielektroniki katika shule mbalimbali sambamba na usambazaji wa vifaa kama kompyuta.
Katika hatua nyingine, Tanzania inaonyesha namna inavyojiandaa kuondokana na mfumo wa urushaji matangazo sambamba na kutoa masafa kwa analojia kuelekea digitali, hali ambayo itaongeza uhuru mkubwa kwa watumiaji sambamba na kuwa na fursa nyingi za kupata matangazo kwa wananchi. Mfumo huu unahamasishwa na ITU ambayo pia katika mkutano wa mwaka huu, inahamasisha kuhusu namna njema ya kutumia changamoto zinazotokana na magunduzi ya Brodabendi (Broadband) mfumo unaoongeza kasi ya matangazo ya sauti, data na video katika intaneti.
Mkutano huu wa ITU unafanyika huku Tanzania na dunia ikiwa katika mpango wa kumaliza kabisa mfumo wa analojia ifikapo mwaka 2015. Katika Afrika Mashariki, nchi ya Kenya inaonekana kuongoza kufuatia kuwa tayari na sera ya kuingiza mfumo wa kidigitali lakini hali nchini Tanzania kwa mujibu wa TCRA iko juu na inawezekana kabisa kuwa mfumo huo ukawa umefika maeneo yote nchini kabla ya kuzimwa rasmi na Bodi ya dunia.
Katika mkutano huu pia yupo Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Mbarawa Mnyaa ambaye amehudhuria mikutano kadhaa kwa ngazi ya mawaziri huku akinadi fursa zilizopo katika wizara yake kwa wawekezaji sambamba na kubadilishana uzoefu kuhusu makuzi ya ugunduzi katika sayansi, teknolojia namawasiliano. Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Bilal pia amepata fursa ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya nchi jirani kama Rwanda, 
 
Kenya, Malawi, Ghana, China, Uganda na Burundi. Katika mabanda hayo Makamu wa Rais alijionea na kupata taarifa juu ya umuhimu wa mkongo wa Tanzania unaoziunganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati katika kupata huduma za Intaneti kwa gharama nafuu na pia umuhimu wake katika kuingiza pato kwa Tanzania.

JK ATUA PERTH, AUSTRALIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Perth, Australia, jioni ya leo, Jumanne, Oktoba 25, 2011, kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Madola (Commonwealth Heads of Government Meeting – CHOGM) mwaka huu.

Rais Kikwete akiongozana na Mama Salma Kikwete amewasili mjini Perth tayari kujiunga na viongozi wenzake wa nchi za Jumuia ya Madola kwa ajili ya mkutano uliopangwa kuanza Ijumaa, Oktoba 28, 2011, katika ukumbi wa Riverside Theatre.

Kama ilivyo kawaida, Mkutano huo wa CHOGM ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, umetanguliwa na Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za Nje za Jumuia ya Madola na wakati CHOGM inaendelea itakuwepo mikutano mingine ikiwa ni pamoja na Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Vijana, Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Biashara na Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Wananchi .

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Rais Kikwete kuhudhuria Mkutano wa CHOGM tokea ashike madaraka ya kuongozwa Tanzania miaka sita iliyopita. Alishiriki mikutano ya CHOGM iliyofanyika mjini Kampala, Uganda, mwaka 2007, na mjini Port of Spain, Trinidad na Tobago, mwaka 2009.

Mbali na kuhudhuria Mkutano wa CHOGM, Rais Kikwete atatumia nafasi ya Mkutano huo kukutana na viongozi mbali mbali wa nchi na mashirika ya kimataifa ya sekta za umma na sekta binafsi.

Miongoni mwa shughuli zake za kwanza kesho, Rais Kikwete anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Jumuia ya Watanzania wanaoishi katika eneo la Australia Magharibi.
Keshokutwa, Rais Kikwete atakuwa mzungumzaji katika mdahalo kuhusu jinsi ya kuwawezesha akinamama ili waweze kuongoza – Empowering Women to Lead- ulioandaliwa na Mheshimiwa Julia Gillard, Waziri Mkuu wa Australia na mwenyeji wa CHOGM mwaka huu baada ya ameshikiri katika halfa kuhusu suala hilo hilo itakayoandaliwa na Mheshimiwa Quetin Bryce AC, Ganava Mkuu wa Australia (The Commonwealth of Australia).

Keshokutwa hiyo hiyo, Rais Kikwete pia atakuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Jumuia ya Madola wa Biashara ambako atatoa hotuba maalum yenye mada: “Africa: Creating a New Economic Power for the 21st Century”. Siku hiyo hiyo, Rais Kikwete atakuwa mwenyekiti wa mkutano kuhusu suala la madini kati ya Tanzania na Australia wa “Tanzania-Australia Mining Roundtable” ambao utahudhuriwa na baadhi ya wafanyabiashara.

Miongoni mwa mambo makubwa yatayojadiliwa kwenye Mkutano wa CHOGM mwaka huu ni pamoja na viongozi wa nchi wanachama wa Jumuia kuangalia jinsi ya kuimarisha uwezo wa Jumuia katika kuunga mkono demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora miongoni mwa nchi wanachama waa Jumuia hiyo.

Mkutano huo pia utajadili jinsi ya nchi wanachama wanavyoweza kukabiliana na changamoto za sasa za kimataifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uchumi endelevu, jinsi ya kuondokana na matatizo za sasa ya kiuchumi duniani na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano pia utajadili changamoto za usalama wa chakula duniani, maendeleo endelevu na menejimenti ya maliasili.
 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
     Zanzibar                                                                                               25.10.2011
FINLAND imeeleza azma yake ya kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuendeleza Mradi wa  kutunza mazingira hapa Zanzibar (SMOLE).
 
Balozi wa Finland nchini Tanzania Mhe.Sinikka Antila aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungunzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
 
Katika mazungumzo hayo, balozi huyo wa Finland alimueleza Dk. Shein kuwa  Finland inathamini sana mashirikiano yaliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa nchi yake itahakikisha inaendelea kuunga mkono mradi wa SMOLE hapa Zanzibar.
 
Alisema kuwa   Finland ni nchi inayotajika na iliyopiga hatua kubwa katika masuala ya uhifadhi mazingira na misitu duniani hali ambayo ilisaidia kuinua uchumi wa nchi hiyo na  kueleza haja kwa Zanzibar ya kutunza mazingira kwani yanaweza kusaidia uchumi.
 
Balozi Antila alisema kuwa Finland imeanza kushirikiana na Zanzibar katika masuala ya uhifadhi mazingira na misitu kwa muda mrefu hivi sasa.
 
Alisema kuwa katika awamu ya pili ya mradi wa SMOLE ambao umeanza Julai 2010 hadi June 2013, nchi yake imetoa zaidi ya bilioni 8 katika kuhakikisha maendeleo ya mradi huo yanafikiwa.
 
Aidha, alieleza kuwa licha ya changamoto mbali mbali zikiwemo usajili wa ardhi, Balozi huyo alieleza kuwa anamatumaini makubwa ya mafanikio juu ya mradi huo na kusisitiza kuwa miongoni mwa madhumuni ya mradi huo ni kupambana na umasikini, kutunza mazingira na maendeleo ya kiuchumi.
 
Pamoja na hayo, balozi huyo alimueleza Mhe. Rais juu ya matarajio ya kuja Zanzibar Waziri anayeshughulikia masuala ya mazingira wa Nchi hiyo hapa Zanzibar hivi karibuni.
 
Nae Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Balozi huyo kutokana na ujio wake na kumueleza kuwa Finland ina historia kubwa katika mashirikiano na Zanzibar juu ya masuala ya mazingira na misitu.
 
Alieleza kuwa Finland imekuwa na mashirikiano mazuri na Zanzibar hatua ambayo imeweza kuisaidia Zanzibar katika masuala mazima ya mazingira sanjari na ujuzi ya masuala hayo.
 
Alisema kuwa Finland ni nchi ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa juu ya masuala ya mazingira hatua ambayo ilizipelekea nchi nyingi za Afrika kuja kufuata ujuzi hapa Zanzibar na kueleza kuwa kutokana na kuona umuhimu wa mazingira ndipo akachukua hatua za makusudi kuweka sekta hiyo chini ya Afisi ya Makamu wa Kwanza  wa Rais.
 
Dk. Shein pia, alimueleza balozi huyo kuwa kuna haja ya kuimatisha uhusiano kati ya Zanzibar na Finland katika sekta ya elimu, uhifadhi wa mazingira na mafunzo mengine muhimu juu ya mazingira na ardhi.
 
Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuitangaza zaidi Zanzibar nchini mwake katika medali ya Utalii pamoja na uwekezaji ambapo Balozi huyo wa Finland aliahidi kuifanya kazi hiyo ipasavyo.
 
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania anaemaliza muda wake wa kazi Mhe. Fatuma Ndangiza, Ikulu mjini Zanzibar.
 
Katika mazungumzo yao viongozi hao walieleza azma ya kushirikiano katika kuimarisha sekta za maendeleo kati ya Zanzibar na Rwanda ikiwemo sekta ya utalii, elimu ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na wakufunzi kwa vyuo vikuu vya SUZA na Kigali, utamaduni, mazingira na sekta nyenginezo.
 
Balozi Ndangiza alimpongeza Dk. Shein kwa mafanikio yaliopatikana Zanzibar kutokana na uchaguzi uliokuwa huru na haki na baadae kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni hatua ya kupigia mfano na kueleza matumaini yake ya kupatikana maendeleo endelevu hapa Zanzibar kutokana na uongozi imara wa Dk. Shein.
 
Mhe Ndangiza alimueleza Dk. Shein kuwa Rwanda imeona ipo haja ya kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya Utalii ambapo inatarajia kuanzisha safari za ndege kwa kutumia Shirika lake la ndege la nchi.
 
Katika mazungumzo hayo naye Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa hatua ya Shirika la ndege la nchi hiyo kutasaidia ushirikiano huo na kusisitiza Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Rwanda kwa manufaa ya nchi mbili hizo.
 
 Rajab Mkasaba

Monday, October 24, 2011

MAALIM SEIF ASEMA KUNA HAJA KWA WATENDAJI WA SERIKARI KUTEKELEZA KWA HARAKA MAAMUZI YA VIKAO

Maalim Seif akimueleza mwenyekiti wa   Baraza la mpango wa Afrika wa kijitathmini katika utawala bora (APRM) nchini Tanzania Bw. John Shibuda, wakati ujumbe wa Taasisi hiyo ulipofika OMKR Migombani kutoa tathmini ya utafiti wao.
Maalim Seif akisikiliza tathmini ya ripoti ya APRM kuhusu Utawala Bora Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar (Picha: Salmin Said OMKR).


Na: Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuna haja kwa watendaji wa serikali kutekeleza kwa haraka maamuzi yanayofikiwa kwenye vikao vya juu vya kutatua kero za Muungano ili kuondoa malalamiko kwa wananchi.
Maalim Seif amesema hayo leo huko ofisini kwake migombani alipokutana na wajumbe wa Baraza la mpango wa Afrika wa kijitathmini katika utawala bora (APRM) nchini Tanzania waliofika kuwasilisha tathmini  ya utafiti wao.
Makamu wa kwanza wa Rais amesema serikali imeunda kamati ya kutatua kero za Muungano ambayo kwa Zanzibar inaongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, na Tanzania Bara inaongozwa na Waziri Mkuu kwa nia njema, hivyo watendaji hawanabudi kufanikisha azma hiyo kwa kutekeleza yale yanayotolewa maamuzi.
Makamu wa kwanza wa Rais amesema miongoni mwa mambo yaliyofikiwa maamuzi ni pamoja na suala la wafanyabiashara kutozwa kodi katika bandari wanayofikisha bidhaa zao mara ya kwanza, lakini hadi sasa kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara hasa wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.
Amefahamisha kuwa tabia kama hiyo haina budi kukomeshwa, kwa vile inarejesha nyuma juhudi za wananchi kujiendeleza kiuchumi.
Aidha Maalim Seif ameelezea kuwepo utitiri wa taasisi za kukusanya kodi nchini na kutaka kuangaliwa uwezekano wa kupunguzwa kwa taasisi hizo.
katika tathmini yao wajumbe hao wamebainisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na serikali yao juu ya kero za Muungano.
Akizungumzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Mwenyekiti wa taasisi hiyo John Shibuda amesema serikali hiyo imeleta mafanikio makubwa na ni mfano wa kuigwa na Tanzania na nchi nyengine barani Afrika hasa katika nchi ambazo zimekuwa zikikumbwa na migogoro ya kisiasa.
Bw. Shibuda Amesema kuna haja ya ufuatiliaji wa karibu wa utendaji wa serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar, ili uweze kuwa endelevu na kuwasiliana na uongozi wa bunge ili kumuomba Makamu wa kwanza wa Rais kutoa taaluma na uzoefu wake juu ya Serikali hiyo kwa wabunge.
“Wabunge tunahitaji sana kujifunza uzoefu na mafanikio ya serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar”, amesema kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi.
Maalim Seif amesema mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa yamepatikana kutokana na nia njema ya waanzilishi wa maridhiano na wananchi wa Zanzibar kumaliza migogoro na kujiletea maendeleo.
Akizungumzia uchumi na maendeleo Makamu wa kwanza wa Rais amesema bado Zanzibar iko nyuma katika Sekta ya Viwanda na kwamba inahitaji kujiendeleza ili kuweza kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Mbali na Viwanda, Maalim Seif amesema serikali ina nia thabiti ya kuliendeleza zao la karafuu, ili katika kipindi cha miaka kumi ijayo zao hilo liweze kurejeshewa hadhi yake kama ilivyokuwa hap kabla.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amesema serikali inaendelea na mkakati wake wa kuimarisha miundo mbinu ya usafiri ili kuwawezesha wafanya biashara na wawekezaji kufanya shughuli zao bila usumbufu.
“Tatizo letu kwa sasa ni usafiri wa baharini na angani, lakini kwenye barabara tumepiga hatua kubwa. Namshukuru sana Rais mstaafu Dkt Karume kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuimarisha barabara”, amesema Maalim Seif.
Mapema akiwasilisha ripoti ya tathmini ya utafiti wao kuhusiana na utawala bora, Katibu mtendaji wa Taasisi hiyo ya The African Peer Review Machanism (APRM Tanzania) bibi Rehema Twalib lengo la tathmini hiyo ni kujenga fikra endelevu kwa maslahi ya nchi.
Nae mjumbe wa taasisi hiyo Bw. Salim Said amelalamikia uwakilishi mdogo wa wajumbe wa Zanzibar kwenye Taasisi hiyo ambapo kati ya wajumbe 20 Zanzibar ina wajumbe wawili pekee.
Jumla ya nchi 30 za Afrika zinashiriki katika mchakato huo huo wa kujitathmini ambapo kwa kuanzia kila nchi hujitathmini yenyewe na baadae wataalamu wa mpango huo kutembelea kila nchi ili kutoa maoni yao kuhisiana na tathmini zinazotolewa.
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dr. Ali Mohamed Shein, leo ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Jaji Mohammed Chande Othman kuwa Mjumbe na  kushiriki vikao vya Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Hii ni kutokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu 54 ibara ya kwanza ambayo inawataja wajumbe wa Baraza la Mawaziri kuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote.
 
Kiapo hicho kimeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu, Mawaziri na maafisa wengine wa serikali
 
Mara baada ya kula kiapo hicho, Rais Wa Zanzibar amehudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri kikiongozwa na Rais Kikwete.
 
Jioni ya leo, Rais Kikwete anatarajiwa kuelekea Perth, Australia kuhudhuria Kikao cha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola kinachofanyika kuanzia tarehe 28-30 mwezi huu. 
Rajab Mkasaba,  Dar-es-Salaam

WAGONJWA WA MOYO 611 KATI YA 1000 KWENDA INDIA KUFANYIWA MATIBABU YA MOYO

Na Fatma Mzee-Maelezo Zanzibar 24/10/2011

Wagonjwa wa Moyo 611 kati ya 1000 wanatarajiwa kuondoka Zanzibar kwenda nchini India kufanyiwa matibabu ya moyo ambapo kati ya wagonjwa hao wengi wao ni watoto wenye umri chini ya mika kumi na mbili.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Omar Abdalla Ali wakati alipokuwa akimkaribisha Hoyce Temu ambae aliwahi kuwa Mrembo wa Tanzani mwaka 1999 kwa lengo la kuwaona wagonjwa hao ili aweze kuwashawishi watu wenye uwezo kusaidia matibabu ya wagonjwa hao.

Katibu huyo alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali walifanikiwa kuwapeleka wagonjwa 662 nchini Izraeli na wagonjwa 125 kupelekwa India kwa matibabu ya Ugonjwa wa Moyo katika miaka iliyopita.

Aidha aliwataka wadau mbalimbali wenye uwezo kuzidi kulitilia mkazo suala la kuchangi matibabu kwa watu wenye mahitaji ili kuisaidia Serikali katika kukabiliana na matatizo ya kiafya kwa wananchi wake.

Kwa upande wake Mrembo huyo wa Tanzania Hoyce Temu aliwaahidi wazazi wa watoto wenye matatizo ya moyo kuwa atatumia nguvu zake zote kwenda kuwashawishi watu wenye uwezo ili kuhakikisha wanachangia huduma za matibabu kwa wagonjwa hao.

Aidha Hoyce Temu alisema kuwa atarudi Zanzibar baada ya Wiki Moja ili kuleta mchango wowote atakaofanikiwa kuukusanya kutoka kwa wadau mbalimbali ili uweze kusaidia katika Safari ya hiyo ya India.

Amesema atakapo rudi Zanzibar ataanza na safari ya watoto sita ambao watakuwa na hali mbaya zaidi huku wengine wakisubiri kupatikana msaada ili nao wapelekwe huko India.


Aidha Mrembo huyo aliaahidi pia kushirikiana na Madaktari wa Mmanazi Mmoja na wazazi hao ili kuhakikisha tatizo hilo linaweza kupunguwa kwa kiasi kikubwa.

Amewataka Wazanzibari wenye uwezo kulichukulia umuhimu suala hilo ili kuweza kusaidia wanyonge na watu watu wasikuwa na uwezo wa kuwapeleka watoto wao matibabuni.

Nao baadhi ya wazazi wa watoto hao walimshukuru Hoyce Temu kwa ahadi zake na kuwaomba watu wenye uwezo hasa kwa kwa upande wa Zanzibar kusaidia watoto hao kwa hali na mali kwani fungu lao kubwa litabaki kuwa kwa Mungu.

UBALOZI WA UTURUKI NCHINI WATOA MSAADA WA INCUBATORS 10 KWA TAASISI YA WANAWAKE NA MAENDELEO (WAMA)

Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimshukuru balozi wa Uturuki Nchini, Dkt Sander Gurbuz, baada ya kupokea msaada wa mashine 10 za kusaidia watoto waliozaliwa kabla ya muda wao. Mashine hizo, zenye thamani ya dola 30,000 (kama milioni 50), zimetolewa na kampuni ya madini na nishati ya Uturki iitwayo TPM ambapo Mkurugenzi Mkuu wake Bw Burak Buyuksaar (wa tatu kulia) alikuwepo kushuhudisa makabidhiano hayo. Kulia ni mke wa balozi, Mama Durhan Gurbuz. Picha na Ikulu 

Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania umetoa msaada wa incubators 10 zenye thamani ya Tsh. Mil 50/- kwa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Mhe. Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. 

Akikabidhi msaada huo Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Dr. Sander Gurbuz amesema kuwa wametoa msaada huo kwa ajili ya kusaidia moja ya programu za Taasisi ya WAMA inayolenga kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto. Pamoja na kudumisha uhusiano mzuri ambao nchi yake ya Uturuki na Tanzania umekuwa nao.
Mhe. Balozi aliambatana na Mke Wake Mama Durhan Gurbuz na Mkurugenzi Mkuu wa TPM Mining and Energy Co. Limited, Bw. Burak Buyuksarac. 
 
Akitoa shukrani baada ya kupokea msaada huo Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA, Mhe. Mama Salma Kikwete amesema kuwa msaada huo ni mkubwa sana na utasaidia kuokoa maisha ya watoto wachanga ambao wangeweza kufa kutokana na ukosefu wa vifaa hivi hasa maeneo ya vijijini. Mama Salma aliongeza kuwa pamoja mazingira ya Vijijini yanaweza yasiruhusu sana utumiaji wa vifaa hivi lakini kwa sababu siku hizi kuna umeme wa jua utasaidia matumizi ya vifaa hivi.